HYDERABAD, INDIA
Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb.), Waziri wa Uchukuzi ameshiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga yanayojulikana kwa jina la Wings India 2024.
Maonesho hayo ambayo yameandaliwa na Wizara ya Usafiri wa Anga, India kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda nchini India (FICCI) na yanafanyika katika uwanja wa ndege wa Begampert, mjini Hyderabad, India tarehe 18-21 Januari 2024.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri ameambatana Bw. Hamza Saidi Johari- Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Dkt. Kheri Omari Goloka- Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini India.
Katika ziara hiyo, tarehe 18 Januari 2024 Mheshimiwa Waziri Mbarawa ameshiriki katika sherehe za ufunguzi wa maonesho ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga nchini India (Wings India 2024) pamoja na kutembelea mabanda ya maonesho hayo, kujionea teknolojia za kisasa katika sekta ya usafiri wa anga; na kupata maelezo ya shughuli za usimamizi na uendeshaji wa masuala ya usafiri wa anga nchini India.
Vilevile Waziri Mbarawa amekutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa Usafiri wa Anga wa nchini India na wanaotoka katika mataifa mbalimbali duniani. Miongoni mwa wadau waliofanya mazungumzo na Mhe. Waziri ni Kampuni ya GMR Aerospace and Industrial Park ya nchini India ambayo ni kampuni binafsi inayojihusisha na Ujengaji, Uendelezaji na Uendeshaji wa Viwanja vya Ndege kwa utaratibu wa PPP.
Aidha, Katika Vikao maalum Mheshimiwa Profesa Mbarawa amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Jyotiraditya Scindia, Waziri wa Usafiri wa Anga, Jamhuri ya India. Katika kikao hicho masuala yafuatayo yalizungumzwa na kukubalika:- Kujenga Uwezo wa Wataalam katika Masuala ya Usafiri wa Anga (Training and Capacity Building in Civil Aviation). Wizara ya Usafiri wa Anga nchini India na Wizara ya Uchukuzi Tanzania zimekubaliana kuwa na mashirikiano katika mafunzo ya Usafiri wa Anga hususani Tanzania kupeleka wanafunzi nchini India watakaopata mafunzo ya muda katika fani za Urubani (Pilot) na Uhandisi wa Ndege (Aircraft Maintenance Engineering); Kufanyika mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya Uendelezaji na Uendeshaji wa Viwanja vya Ndege kwa utaratibu wa PPP kwa kushirikisha sekta binafsi.
Katika hatua zaidi ya kuboresha mashirikiano ya Usafiri wa Anga baina India na Tanzania, Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Mbarawa ameilekeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ianze mchakato wa kupitia Bilateral Aviation Safety Agreement (BASA) iliyopo kati ya India na Tanzania ili iendane na mahitaji ya sasa ya Usafiri wa Anga wa nchi hizi.
0 Comments