Katibu wa chama cha ushirika cha wavuvi na wachuuzi, Mwalo wa Deep Sea Wilaya ya Tanga Bahero Adhio.
Boti ya kisasa waliyopatiwa chama hicho na serikali kwa mkopo wa masharti nafuu bila riba.
*************************
NA Hamida Kamchalla, TANGA.
WAVUVI wadogo wadogo kupitia Chama cha Ushirika Deep Sea wilayani Tanga wameendelea kunufaika, baada ya serikali ya awamu ya sita kuwapatia boti kubwa ya kisasa iliyogharimu sh milioni 121 kwa lengo la kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa tija zaidi.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi na Wachuuzi katika mwalo wa Deep Sea Wilaya ya Tanga, Bahero Adhio ametoa taarifa hiyo ofisini kwake mtaa wa Chumbageni.
Katika mazungumzo yake hayo, Adhio amesema kwamba serikali kupitia Benki ya Kilimo nchini imetoa zana hizo za uvuvi ambapo wavuvi watahitajika kufanya marejesho pasipo na riba.
"Serikali imetoa zana nzuri za uvuvi, sisi wilaya ya Tanga tumepata fible boat kubwa HP 75 mita 14 inayogharimu sh milioni 116 ukichanganya na bima na thamani ya dola ndio 121 milioni "amesema.
Adhio amebainisha kwamba, kupatikana kwa msaada huo kutawawezesha wavuvi kutoka kwenye uvuvi mdogo wa kuvua karibu na sasa watakwenda kina kirefu.
"Chama chetu cha ushirika Deep Sea kimepewa boat ya kisasa, imetolewa na serikali kupitia Benki ya Kilimo iliyowakopesha wavuvi zana bila riba na marejesho ni baada ya miaka mitano" amesema Adhio.
Adhio mbaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Wilaya ya Tanga (CHAWAWATA) amesema, wameendelea kuwaelimisha wavuvi kujua mipaka yao kiutendaji sanjari na kuwaasa matumizi ya zana zisizohitaiika katika uvuvi.
Pia amesema kwamba, Sera za CHAWAWATA ni kuunganisha wavuvi wadogo wadogo hususani vijana hatua ambayo inasaidia kutoa fursa kwao kupatiwa usaidizi.
Kwa mujibu wake uwepo wa chama cha wavuvi umesaidia kupata utatuzi juu ya kero mbalimbali zinazowakabili hatua ambayo pia imetoa urahisi kutambulika na Wizara yao.
Ameongeza kusema kuwa, kupitia chama chao wameanza kufanya mawasiliano na Mamlaka zinazohusika na kada yao kuangalia jinsi gani wavuvi watakavyo shirikishwa kwenye mambo ya kisheria kabla ya sheria zinazowahusu kutekelezwa.
0 Comments