Na. Alfred Mgweno (TEMESA RUVUMA)
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Elias Thomas ameutaka uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha unaacha kujifungia ndani na unazitembelea na kushirikiana kwa karibu na Taasisi zote zilizoko Mkoani humo ili ziweze kulipia madeni ambayo Wakala unazidai.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wadau wanaotumia huduma za Wakala huo katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chandamali ulioko mjini Songea. Kikao kilichohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Wakurugenzi wa Wilaya pamoja na wakuu wa Taasisi zilizoko Mkoani Ruvuma, wauzaji wa vipuri, wamiliki wa gereji binafsi pamoja na washitiri kutoka mashirika mbalimbali Mkoani humo.
‘’TEMESA mnahudumia Taasisi za Serikali, tokeni, mpite muende kwenye zile Taasisi mnazozihudumia, zungumzeni nao, mjuwe ziko wapi, mjue wana changamoto gani, mshauriane nao ili muone ni jinsi gani ya kuweza kulipa yale madeni mnayowadai lakini muweka nao mpango mkakati mzuri wa kutengeneza magari yao.’’ Amesema Mhe Kanali Laban.
Mkuu wa Mkoa pia amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha TEMESA Mkoa wa Ruvuma, kwanza kuwa na karakana ambayo inatembea (Mobile Workshop), lakini vilevile kuchukua jukumu la kujenga na kukarabati karakana ya Mkoa huo.
‘’Mhe. Raisi yeye ameshamaliza jukumu lake iliyobaki ni jukumu letu sisi, lakini na sisi hatulipii huduma tunazopatiwa na TEMESA kwa wakati, kwa taarifa niliyonayo, wateja wa Mkoa wa Ruvuma wanadaiwa na TEMESA si chini ya shilingi Bilioni 1.5, na ndio maana wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na wasaidizi wenu tumewaita hapa, nyinyi ndio wadau wakubwa wa Taasisi hii, na nyinyi ndio wenye magari, ni wajibu wetu sisi ambao tunapatiwa huduma TEMESA kulipa madeni hayo kwa wakati na hatuna sababu yoyote ya kupeleka magari yetu nje ya TEMESA.’’ Alisema Mkuu wa Mkoa.
Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Hassan Karonda ambaye amemuwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, akizungumza katika kikao hicho, amesema lengo la kikao hicho ni kuuleta Wakala huo karibu na wadau wake, kupokea maoni, ushauri pamoja na kutoa mrejesho wa yale ambayo Wakala huo umeahidi kuyatekeleza ili kuboresha huduma kwa wateja wake.
’’Sasa hivi tumeanza kupata vifaa vya kisasa hivyo tunaishukuru sana Serikali, karakana zetu zimeanza kufanyiwa ukarabati mkubwa, mafundi wetu wameanza kupatiwa mafunzo kama mnavyofahamu Teknolojia inabadilika kila siku, hivyo tunawapelekea mafundi wetu kwenye mafunzo ili kuwapatia ujuzi waweze kutengeneza magari ya kisasa kwa ufanisi mkubwa zaidi.’’ Amesema Mkurugenzi.
Mhandisi Karonda ametumia pia fursa hiyo kutoa wito kwa Taasisi za Serikali Mkoani Ruvuma pamoja na Nchi nzima kuhakikisha wanalipia huduma wanazopatiwa na Wakala huo kwa wakati ili kuuwezesha Wakala kuendelea kutoa huduma kwa ubora na ufanisi.
‘’Hata kitu kikiwa kizuri namna gani, kama hutaweza kukilipia na kukitunza vizuri hakiwezi kuwa endelevu, kwahiyo tumeona tumeingia mikataba na wenzetu hawa, tumepeleka mafundi wetu kwenye mafunzo, tunajitahidi kuweka utaratibu mzuri wa matengenezo, lakini bila ya nyinyi ambao mnatuweka mjini kulipia madeni na kulipia kwa wakati, hatuwezi kutoa huduma iliyo bora’’ Amemaliza Mhandisi Karonda.
Mhandisi Karonda pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kukubali kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji TEMESA na kwa kuendelea kutenga fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa karakana mpya, kununua vitendea kazi pamoja kukarabati karakana za Wakala huo katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Tanga, Lindi, Mtwara, Mara, Arusha, Tabora pamoja na Kigoma huku akiahid kwamba juhudi hizo za Serikali hazitapotea na Wakala utafanya kazi kwa weledi na ufanisi ili juhudi hizo zinazotolewa na Serikali zisipotee bure.
Awali, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi kutoka TEMESA Bi. Josephine Matiro akizungumza katika kikao hicho amesema, Kikao cha Wadau Mkoa wa Ruvuma kinakuwa ni cha Ishirini tokea Wakala huo uanze utaratibu wa kukutana na wadau wake, amesema uwepo wa vikao hivyo umeuwezesha Wakala uanza kufanya mabadiliko makubwa. ‘’Kusema ukweli viko hivi vimeonyesha tija kubwa, kutokana na vikao hivi tumeanza kufanya mabadiliko, mmeona vifaa pale nje, juhudi ambazo Serikali yetu inafanya kuiboresha TEMESA ili iweze kutoa huduma bora na yenye tija kwa Taasisi za Serikali na binafsi. Amesema Bi Matiro.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Elias Thomas (wa
pili kulia aliyevaa koti na shati jeupe) akikagua baadhi ya vitendea kazi
vinavyotumika katika karakana ya TEMESA Mkoa wa Ruvuma wakati alipohudhuria
kikao cha wadau wanaotumia huduma za Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania
(TEMESA) Mkoa wa Ruvuma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za
Ufundi Mhandisi Hassan Karonda na Meneja wa TEMESA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi
Frank Msyangi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Elias Thomas
katikati akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wanaotumia huduma za
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) mara baada ya kufungua rasmi kikao
cha wadau hao Mkoani RUVUMA kilichofanyika katika ukumbi wa Chandamali leo.
0 Comments