****
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameipongeza kampuni ya Dhahabu ya Barrick, ambayo inaendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation kwa kufanya uwekezaji wenye tija na ufanisi ambao umeanza kuleta mabadiliko chanya kwa kuchangia pato la Taifa sambamba na kufanikisha miradi mbalimbali ya kijamii na kuongeza wigo wa ajira kwa watanzania.
Dkt. Kiruswa alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali wakati wa mkutano ulioandaliwa na Barrick kwa ajili ya kutoa taarifa za utendaji wa kampuni katika kipindi cha robo mwaka uliopita kwa waandishi wa habari na wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa Barrick Bulyanhulu ambao pia ulijumuisha viongozi wa Serikali.
Alisema ubia wa Serikali na kampuni ya Barrick umekuwa ukiendelea kupata mafanikio siku hadi siku na mchango wa faida inayotokana na ubia huu kuingia katika mfuko wa Serikali na huduma za kijamii kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka migodi ya Barrick kupata huduma bora kupitia miradi inayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR).
"Serikali tunajivunia uwekezaji huu ambao ni mfano wa kuigwa pia natoa wito kwa makampuni ya wawekezaji kuwa na programu za kukutana na viongozi wa Serikali katika maeneo yao na kutoa ripoti za utendaji,hii mbali na kudumisha uwazi inachangia kupata maoni ya wadau kutoka pande zote mbili", alisisitiza, Dkt. Kiruswa.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow akiongea katika mkutano huo, kushoto kwake ni Meneja wa Barrick nchini, Melkiory Ngido.
Kwa upande wake, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema kuwa migodi ya Dhahabu ya Barrick ya North Mara na Bulyanhulu imeendelea kudumisha rekodi yake ya utendaji mzuri na kufikia mwongozo wa uzalishaji kwa mwaka 2023.
Alisema mageuzi ya migodi miwili iliyokuwa imetelekezwa kuwa mkusanyiko wa maeneo ya uchimbaji wenye hadhi ya kimataifa ambayo kwa pamoja inazalisha dhahabu katika kiwango cha daraja la kwanza,yanaonesha mafanikio yanayoweza kufikiwa pale kampuni za uchimbaji madini na Serikali wenyeji zinaposhirikiana katika kuwapatia wadau wao thamani halisi.
“Ubia wa Twiga sio tu kwamba umeleta mageuzi katika tasnia ya uchimbaji wa dhahabu nchini Tanzania bali pia umeiweka nchi, inayojulikana kama kivutio cha utalii barani Afrika,katika nafasi ya kivutio kikuu cha uwekezaji ambacho kina utajiri mkubwa wa raslimali za chuma na madini,” alisema Bristow.
Uchimbaji wa kupekecha katika migodi yote miwili unaonyesha mafanikio katika hifadhi zake za dhahabu zilizokuwa zimeishiwa au kupungukiwa dhahabu. Katika mgodi wa North Mara, uwezekano wa kuwa na shughuli nyingine za uchimbaji chini ya ardhi unachunguzwa huku uboreshaji wa mpango wake wa mgodi wa wazi unatarajiwa kuongeza miaka zaidi katika uhai wake, katika mgodi wa Bulyanhulu, kuna fursa karibu na uso wa ardhi na uwezekano wa kuongeza uzalishaji na kunyumbuka kwa uchimbaji.
Bristow, alisema tangu Barrick ichukue migodi ya Tanzania mwaka 2019 imekua na kuwa mchangiaji mkubwa wa mapato ya Serikali, kupitia kodi, ajira, malipo kwa wazabuni wa ndani, miradi ya jamii na gawio kwa wanahisa.
Uwekezaji wake katika uchumi hadi sasa una jumla ya zaidi ya dola bilioni 3.4 (kwa msingi wa 100%), ambapo kutokana na mafanikio haya migodi yake katika kipindi cha mwaka jana imetunukiwa tuzo mbalimbali za utendaji kazi kwa ufanisi mkubwa.
Awamu ya kwanza ya mpango wa Twiga wa kusongesha Mbele mustakabali wa Elimu ( Twiga Future Forward Education Initiative) wenye thamani ya Dola milioni 30 inakaribia ukingoni. Mpango huu utaboresha kwa kiasi kikubwa miundombinu ya elimu ya Tanzania kwa kutoa vyumba vya madarasa,mabweni na vyoo kwa wanafunzi zaidi wapatao 49.000.
Kwa upande wao Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme na Mkuu wa mkoa Geita, Martin Shigella, wakiongea kwa nyakati tofauti katika mkutano huo walipongeza kampuni ya Barrick kwa kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika mikoa yao hususani kupitia miradi inayotekelezwa na fedha za uwajibikaji kwa jamii ambayo imeboreha sekta mbalimbali hususani afya ,elimu ,maji safi na miundombinu ya barabara.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella akiongea katika mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita akitambulisha viongozi wa mkoa katika mkutano huo
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akishirikiana na Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga na Christina Mndeme kukikabidhi mfano wa hundi zenye thamani ya dola 10,000 kwa viongozi wa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusiha na kupambana na changamoto mbalimbali katika jamii. Fedha hizo zimetolewa na taasisi ya NVeP inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow (pichani mwenye kofia). Mashirika 5 yasiyo ya kiserikali yamefanikiwa kupata msaada huo katika awamu hii ya robo ya mwaka.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, akishirikiana na Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga na Christina Mndeme kukikabidhi mfano wa hundi zenye thamani ya dola 10,000 kwa viongozi wa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusiha na kupambana na changamoto mbalimbali katika jamii.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, akishirikiana na Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga na Christina Mndeme kukikabidhi mfano wa hundi zenye thamani ya dola 10,000 kwa viongozi wa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusiha na kupambana na changamoto mbalimbali katika jamii.
0 Comments