WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua na kukabidhi mradi wa matundu 12 ya vyoo, sehemu ya kunawia mikono, chumba maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji, chumba maalum kwaajili ya wasichana kujisitiri, pamoja na sehemu ya kuchomea taka hususani taulo za kike zilizokwisha kutumika uliotekelezwa na Taasisi ya Flaviana Matata kwa ufadhili wa SEGAL FAMILY FOUNDATION na MFADHILI MWINGINE, katika shule ya sekondari Manyunyu iliyopo mkoani Njombe.
Mradi huo utanufaisha jumla ya wanafunzi takribani 910 kila mwaka katika shule ya sekondari Manyunyu na sambamba na hilo miundombinu hiyo itatatua changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa vyoo,kichomea taka na upatikanaji wa maji shuleni hapo.
Hafla ya Uzinduzi huu imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Flaviana Matata, Bi. Flaviana Matata akiambatana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Njombe akiwemo Mkuu wa Mkoa, DAS , Mkurugenzi wa halmashauri , pamoja na mashirika na wadau mbalimbali ambao wanatekeleza miradi ya maji na usimamizi wa usafi ya WASH nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa njia ya simu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda ameipongeza Taasisi ya Flaviana Matata kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa kwenye sekta ya elimu hasa katika maeneo ambayo yamekuwa na changamoto .
"Nimefurahi sana kuendelea kushuhudia kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Taasisi hii chini ya mkurugenzi wao Ms. Flaviana na tunaendelea kuona matokeo chanya yanayoendelea katika maisha ya wanafunzi hususani mabinti. Upatikanaji wa huduma bora za usafi wa mazingira ni haki ya msingi kwa kila mtu na ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa wanafunzi wana rasilimali wanazohitaji ili kufaulu kielimu na kuishi maisha yenye afya". Amesema Prof. Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda amewahamasisha wanafunzi wa shuele ya Manyunyu kutia juhudi kwenye masomo yao ili kuwatia moyo na kuongeza kasi kwa wadau kama Flaviana Matata Foundation.
Kwa upande wake Mwanzilishi wa Taasisi hiyo Bi. Flaviana Matata amesema msaada unaotolewa na Flaviana Matata Foundation ni muhimu, kwa kutanguliza mahitaji ya usafi wa mazingira kwa wasichana mpango huo sio tu unaunda mazingira bora na safi lakini pia unaondoa vikwazo vinavyowazuia kuendelea na elimu yao.
"Tunaamini kwa kuendelea kutatua changamoto hizi kutachochea mabadiliko chanya sasa na kwa miaka ijayo". Amesema Bi. Flaviana Matata.
Katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Elimu maalum Tanzania Dkt . Magreth Matonya alishiriki kama mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda ambapo nae aliipongeza taasisi ya Flaviana Matata kwa kazi nzuri wanazoendelea kufanya katika mikoa tofauti nchini.
0 Comments