Ticker

6/recent/ticker-posts

WALIMU SOMO LA HISTORIA WATAKIWA KULINDA NA KUFUNDISHA MISINGI NA MAADILI YA HISTORIA YA NCHI

Mtendaji Mkuu wa Chuo Cha ADEM, Dkt. Siston Masanja akizungumza wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa ambapo amemuwakilisha katika Kongamano la Chama Cha Historia Tanzania lililofanyika leo Desemba 15,2023 Jijini Dar es Salaam.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WALIMU wa somo la historia watakiwa kulinda na kufundisha misingi na maadili ya historia ya Taifa la Tanzania inayochochea Umoja na mshikamano unaoamsha na kukuza moyo wa uzalendo kwa wananchi katika kipindi Cha utandawazi na taifa linapokua katika maendeleo ya kiuchumi,kijamii na Sayansi na Teknolojia.

Rai hiyo imetolewa leo Dec 15,2023, kwenye Kongamano la Chama Cha Historia Tanzania katika ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Chuo Cha ADEM, Dkt. Siston Masanja akimwakilisha Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa.

Amesema wakufunzi wa historia wanawajibu mkubwa wa kutumia elimu yao na utaalamu wao katika ujenzi wa taifa kwa kurithisha moyo wa uzalendo kwa jamii kwa kizazi cha Sasa na kijacho

"Tunategemea wana historia mtumie taaluma na utaalamu wenu kufanya mambo kadhaa ikiwemo kutoa maelezo sahihi kuhusu mchakato wa ujenzi wa taifa na uzalendo, kuhifadhi historia ya jamii zetu na taifa kwa usahihi,kuchochea fikra tunduizi katika masuala ya kitaifa na kimataifa na kimataifa kwa kuzingatia ushahidi halisi wa kihistoria na kutoa tafsiri sahihi wa historia ya Tanzania inayo chochea Umoja na utambulisho wa Taifa"Dkt.Masanja Amesema.

Ameeleza kuwa anatamani kuona Chama cha historia kikiendelea kuchochea mapinduzi katika ufundishaji na Ujifunzaji kwa mtu mmoja mmoja wa somo la historia,na ujenzi wa taifa pamoja na kukuza moyo wa uzalendo miongoni mwa watanzania.

Aidha ameeleza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kipindi Cha mchakato wa mabadiriko ya mtaala wa elimu imegusa maeneo mengi ambayo yanahusiana na somo la historia ambapo wameondoa changamoto ya kujirudiarudia kwa maudhui katika ngazi za shule ya msingi na sekondari.

"Somo litajikita zaidi katika kufundisha historia ya Tanzania,Afrika na dunia kwa ujumla wake,tumeanzisha somo jipya linalo itwa historia ya Tanzania na maadili,somo hili litasomwa katika ngazi zote za Elimu,Elimu ya awali,Elimu ya msingi,Elimu ya sekondari na vyuo vya ualimu litakua ni somo la lazima kwa kila mtoto kwa mfumo wa elimu wa Tanzania"Dkt Masanja Amesema.

Kwa upande wake rais wa Chama cha historia Tanzania Dkt.Oswald Masebo amesema miongoni mwa mada watakazo jadili katika kongamano hilo ni pamoja na fursa na changamoto katika ufundishaji na Ujifunzaji wa somo la historia, mabadiriko katika mtaala wa historia na mahitaji yake,utafiti wa kihistoria na Uandishi wa historia inayo hitajika kwa nyakati za sasa, umuhimu wa historia katika kukuza uzalendo, maadili na utaifa,misingi ya falsafa ya somo la historia ya Taifa la Tanzania na maadili, umuhimu wa historia katika ulinzi usalama na nguvu ya Taifa la Tanzania na historia ya Tanzania baada ya Uhuru.

Aidha amesema kuwa chama Cha historia kinahitaji kuwa na mipango mkakati wa miaka kumi angalau kwa ajili ya kuhakikisha chama kinatanua wigo katika kila pembe ya nchi,na kutoa machapisho yanayo tokana na makongamano hayo ambayo yatachangia kuongezea ufahamu kwa walimu shuleni na rejea vyuoni.

"Chama kinahitaji kuwepo katika kila mkoa,kila wilaya hili bado hatujafanikiwa pia,japo lipo kikatiba mkutano wa leo unaweza kujadili mbinu na mikakati itakayo tumika kukisambaza chama"Dkt.Oswald Amesema.

KONGAMANO hilo limebeba kauli mbiu isemayo FURSA NA CHANGAMOTO KATIKA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA SOMO LA HISTORIA ambapo itakwenda kuibua na kujenga moyo wa kizalendo kwa watu ,kwa ajili ya usalama wa taifa na maendeleo ya nchi.
rais wa Chama cha historia Tanzania Dkt.Oswald Masebo akizungumza  katika Kongamano la Chama Cha Historia Tanzania lililofanyika leo Desemba 15,2023 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments