Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwepo Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ameamua kufupisha safari hiyo na kurejea nchini kwa kushughulikia kwa karibu janga la mafuriko mkoani Manyara.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo imeeleza kuwa Rais Samia ametoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba huo na anawahakikishia wananchi walioathirika kuwa serikali iko pamoja nao na itahakikisha inashughulikia masuala yote yaliotokana na janga hili.
Hata hivyo Idadi ya vifo vilivyosababishwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara sasa ni zaidi ya vifo 50 huku majeruhi waliopelekewa katika hospitali mbalimbali wilaya, mkoa na vituo vya afya ni zaidi ya 80.
Taarifa hiyo ya Ikulu ya Tanzania imeeleza kuwa Maafa haya yameathiri mji wa Katesh hususan vijiji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta na pia vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay, na Sebasi.
"Kwa taarifa za awali nyumba na mifugo imeathirika sana huku idadi za kaya ziliwathirika ni 1,150, idadi ya watu walioathirika hadi sasa ni 5,600 na pia ikikadiriwa takriban ekari 750 za mashamba zimeharibika" imeeleza taarifa hiyo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa serikali igharamie mazishi ya wote waliopoteza maisha kutokana na mvua kubwa iliyotokea na mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.
Rais Samia pia ametaka majeruhi wote ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za Serikali, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kutoa msaada wa dharura na uokoaji.
Aidha Rais Samia ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao.
0 Comments