Na; Mwandishi Wetu – Bujumbura, BURUNDI
Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi/Jua Kali yameendelea kufungua fursa za masoko ya wajasiriamali nje ya nchi na hususan masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ameyasema hayo aliposhiriki ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika jiji la Bujumbura nchini Burundi ambayo yamefunguliwa rasmi leo Desemba 8, 2023 na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Prosper Bazombanza.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa maonesho hayo yamewezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kutambulika kimataifa huku ameshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wajasiriamali 259 kwenda Burundi kutangaza bidhaa na huduma zao.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amewahimiza Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu kutumia fursa ya maonesho hayo kujiajiri na kuondokana na umaskini.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa amewahamasisha wajasiriamali kutumia fursa ya maonesho hayo ili kutangaza bidhaa za Tanzania, kukuza ujuzi na masoko ya bidhaa zao pamoja na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wajasiriamali walioshirikia maonesho hayo wamesema wamepata masoko ya bidhaa wanazozalisha katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
0 Comments