Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amefungua Kongamano la 15 la Umoja wa Vijana Wakatoliki wa Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu Tanzania (TMCS) Taifa, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufungua kongamano hilo leo Mhe. Katambi ameushukuru uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mwanza pamoja na uongozi wa Wanafunzi Wakatoliki Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwa ni pamoja na kuandaa makongamano yenye lengo la kushirikisha vijana katika mambo mbalimbali ya kiimani, kiuchumi na kijamii.
Kupitia Kongamano hilo, Mhe. Katambi amewaeleza Vijana mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kuhusu masuala ya Vijana na Ajira.
"Fursa hizo ambazo zimeendelea kubuniwa ili kuhakikisha Vijana Nchini wanapata fursa mbalimbali ambazo zitawanyanyua kiuchumi ikiwemo Programu ya Building a Better Tomorrow BBT ambapo Vituo Atamizi 13 kwa ajili ya kuwapa vijana ujuzi katika kilimo vimeanzishwa ambapo vijana 812 wamenufaika na mafunzo ya kilimo biashara. Aidha, kwa upande wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi jumla ya Vituo Atamizi nane (8) vyenye jumla ya vijana 238 vimeandaliwa na vijana wanaendelea na mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo",amesema Katambi.
Mhe. Katambi amesema pia Serikali imeboresha Mwongozo wa Utoaji Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) ambapo kwa sasa mikopo inatolewa kwa mtu mmoja mmoja na hadi kufika Januari, 2024 jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 12 zitakuwa zimetolewa.
Aidha kupitia programu Ukuzaji Ujuzi jumla ya vijana 134,093 wamenufaika kupitia mafunzo ya Uanagenzi.
"Vile vile, tumekamilisha maandalizi ya Vijana 6,000 watakaoanza mafunzo ya uanagenzi awamu ya sita katika vyuo 42 nchini na yataanza Januari, 2024 ambapo serikali itatumia kiasi cha fedha kitakachotumika ni shilingi 2,700,000,000 kugharamia mafunzo hayo",ameongeza Katambi.
"Serikali imeendela kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana ambapo Halmashauri 176 zimetenga maeneo yenye ukubwa wa ekari 274,047.33 na Mita za Mraba 540,642.50 kwa ajili ya shughuli za vijana za kiuchumi ambapo jumla ya vijana waliofaidika ni 193,053",ameeleza Mhe. Katambi.
"Hali kadhalika, Serikali imeweza kuboresha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 iliyofuta Sheria ya mwaka 2011. Sheria hii mpya inaendelea kutoa upendeleo kwa makundi ya vijana, wanawake, Wenye Ulemavu na Wazee kushiriki katika mchakato wa manunuzi ya Umma. Mpaka sasa, Kampuni 118 za vijana zimeundwa na kunufaika na 30% ya sheria ya manunuzi ya umma. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 900 katika bajeti kwa ajili ya kutekeza sheria ya manunuzi", amefafanua.
Mhe. Katambi pia amebainisha kuwa, katika kukabiliana na changamoto ya tatizo la Ajira nchini, Serikali imesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika masuala ya kazi na ajira kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi mbili (2) za kimkakati ambazo ni Serikali ya Saudi Arabia na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu ajira za watanzania katika nchi hizo.
"Ninapenda kuwajulisha kuwa, kupitia hati hizi za makubaliano, tumepata fursa 500 za Vijana katika Kada ya Uuguzi kwenda kufanya kazi katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo maombi hayo yanatumwa moja kwa moja kupitia website ya jobs.kazi.go.tz na mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Disemba, 2023. Niwasihi vijana wanaokidhi vigezo kutumia fursa hiyo na nyinginezo zinazotolewa na Serikali",amesema.
0 Comments