************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MTU mmoja amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya magari matatu kugongana eneo la Mifugo, batabara kuu ya Tanga - Segerajijini Tanga.
Akithibitisha hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi amesema tukio limetokea majira ya sita kasoro usiku wa kuamkia jumamosi ambapo ilihusisha gari aina ya lori Iveco, lenye namba T 320 DLH yenye tela namba T 514 AGW, likiendeshwa na Abdallah Khalid likitokea upande wa wilayani Muheza.
Kamanda amebainisha gari jingine ndogo ni Toyota Lactis namba T 940 EZH ambayo ilitokea Tanga mjini kuelekea barabara ya Muheza, ikiendeshwa na Bakari Salimu ambaye alikuwa nyuma ya gari aina ya Suzuki (Kirikuu) namba T 419 CRJ nayo ikitokea Tanga mjini ikiendeshwa na Michael Shirima.
"Ajali hiyo imesababisha kifo cha dereva aliyekuwa akiendesha gari ndogo yenye namba T 940 EZH, Bakati Salimu ambaye alifariki alipokuwa akikimbizwa hospitalini kwenda kupatiwa matibabu,
"Lakini pia kwenye gari hiyo ndiko walikopatikana majeru ambao walipelekwa kupatiwa matibabu ya awali na imeonesha kwamba hawakujeruhiwa sana ndani ya miili yao" amesema Kamanda Mchunguzi.
Aidha ametaja chanzo cha ajali kuwa ni marehemu kupita fari la mbele yake bila kuchukua tahadhari sehemu ambayo kisheria haikumruhusu kumpita aliyekuwa mbele yake bila ishara yoyote kutoka kwake.
"Kwahiyo alivyopita kabla hajarudi upande wake, akakutana uso kwa uso na lori, hii tunaona kwamba chanzo cha ajali hii ni uzembe wa marehemu huyu ambaye hakufuata sheria barabaranii" amebainisha Kamanda.
Hata hivyo Kamanda ameendelea kutoa wito kwa wanaoendesha vyombo vya moto kuchukua tahadhari kwa umakini ili Mkoa wa Tanga kutokuwa na ajali zinazosababishwa na uzembe.
"Kwakuwa hizi barabara zinatumiwa na wengi kama waenda kwa miguu lakini pia hata wanyama na ndiyo maana kukawekwa usalama barabarani, waendelee kuzizingatia wasizione kama mapambo ama zinawachelewesha safari zao" amesema.
Lakini vilevile Kamanda Mchunguzi amesisitiza kuwa wataendelea kuwa wakali zaidi katika kuwafuatilia madereva wazembe kwakuwa huenda wanafanya mazoea kutokana na faini ndogo wanazotozwa wakifanya makosa.
"Sasa tutaona njia mbadala mbali ya faini ili kuhakikisha tunanusuru maisha ya watu, kwasababu wakati mwengine utakuta madereva wanarudia makosa yaleyale,
"Tumeshawaelekeza askari wetu, wako maeneo yote ili kuhakikisha watu wanafuata sheria na kama wataendelea kupuuza basi wasimlaumu yeyote, wafuate sheria za barabarani na wazingatie sheria bila kushurutishwa" amesisitiza.
0 Comments