Nishati Safi si anasa, kaya zote kufikiwa
Wizara ya Nishati imelenga kuboresha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kutokana na umuhimu wa afya za Watanzania na Mazingira. Inakadiriwa Watanzania zaidi ya asilimia 80 wanatumia vyanzo vya nishati ya kupikia ambavyo si salama na vyenye madhara ya kiafya, kiuchumi na kimazingira.
Akimuwakilisha Mgeni rasmi Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko, wakati wa kukabidhi hundi za takribani Shilingi Bilioni 9 za Kitanzania fedha za ruzuku zinazofadhiliwa na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kupitia mfuko wa CookFund kwa wajasiriamali 44 wanaojihusisha na Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia leo Novemba 17, 2023.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesema, jitihada zinazofanyika zitasaidia kupunguza utegemezi wa Nishati zisizo safi na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alihimiza uwepo wa programu endelevu za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia zinalenga kusaidia Wananchi na kujikwamua katika hali za kiuchumi.
"Kwa kweli kwa niaba ya Wizara tunapenda kuwapongeza Umoja wa Ulaya (EU), kwa mradi huu kabambe wa kuboresha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia, lakini vilevile mradi ambao unachagiza maendeleo katika Sekta ya Nishati nchini," amesema Kapinga.
Aidha, ameongeza kuwa programu hiyo ni muhimu kwa Wizara na washirika kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya fedha ambao kwa pamoja wameendelea kuboresha mnyororo wa thamani kutokana na umuhimu wa Nishati safi ya kupikia kwa ustawi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) Cèdric Merel amesema, suala la Nishati safi ya kupikia lisichukuliwe kuwa ni la anasa na kwamba hitaji hilo lifikie kila kaya bila kujali hali ya kipato kwani inasaidia kuokoa muda, ni rahisi kutumia na inalinda mazingira.
"Maono ya Serikali ni kuhakikisha inafikia lengo lake la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya kupikia mpaka ifikapo mwaka 2033, nishati hii safi ya kupikia pia ipatikane kwa urahisi, na kwa ufanisi na kwa gharama nafuu," Cèdric Merel
Awali, Meneja Mradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la (UNCDF), Emmanuel Muro amesema, utekelezaji wa mradi huo umeingia mwaka wa pili na unalenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na kwamba asilimia 80 ya Watanzania wanahama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo safi na kuwataka wadau kuendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha lengo.
Mradi huo wa Nishati Safi ya kupikia unafadhiliwa na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU), ukitekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali (UNCDF), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati.
Hafla hiyo ya utoaji wa hundi kwa wajasiriamali wa Nishati Safi ya Kupikia (44) imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, Mkuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) Cèdric Merel, Wataalam kutoka (UNCDF) na Wizara ya Nishati.
0 Comments