Kufuatia Taarifa ya ukaguzi uliofanywa na timu ya wataalamu iliyoundwa na Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde kuhusu uchambuzi wa mikataba kati ya Vikundi vya wachimbaji wadogo wa madini na wabia(_technical support_) kwenye leseni za uchimbaji mdogo zilizopo katika eneo la Mwakitolyo mkoani Shinyanga kamati imebaini sehemu kubwa ya maduara hayapo katika hali salama ya uchimbaji.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Timu ya watalaamu Mhandisi Ally Samaje amebainisha kwamba eneo la uchimbaji la mwakitolyo linahitajika kukatwa kwa miamba inayoyoning’inia na kurekekebisha maduara ili wachimbaji wachimbe kwa usalama zaidi na kuongeza uzalishaji kuliko ilivyo hivi sasa.
Sambamba na hapo kamati imebaini kuwa uchimbaji wa pamoja (co-existence) kati ya Wachimbaji wadogo na wabia kupitia muongozo wa uchimbaji utakaosimamiwa na Wizara ya Madini.
Akipokea taarifa hiyo,Waziri Mavunde amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Ndg. Msafiri Mbibo kuhakikisha anasimamia kwa ukaribu urekebishaji wa maduara na maeneo yenye miamba inayoning’inia kwa usalama wa wachimbaji wadogo na kuongeza uzalishaji wa madini.
“Suala la usalama katika maeneo ya uchimbaji ni suala muhimu ambalo lazima tulipe uzito mkubwa.
Naelekeza kwamba katika maeneo yote hapo Mwakitolyo yaliyo chini ya ubia wa msaada wa kiufundi(_technical support_) yarekebishwe dosari zote za kiusalama ili kuwaruhusu wachimbaji wadogo wafanye shughuli za uchimbaji katika mazingira ambayo ni rafiki.
Nataka pia niwahakikishie kwamba Hakuna mchimbaji mdogo yoyote atakayeondolewa katika eneo lake kwakuwa eneo hili liligawiwa kwa wachimbaji wadogo kama wanufaika wa kwanza.
Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kuhakikisha tunawasimamia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo ya uchimbaji na pia katika upatikanaji wa mikopo na mitaji ili kuongeza tija katika shughuli zenu”, alisema Mavunde
Mkutano huo wa kupokea taarifa ulihudhuriwa na Viongozi wa Mkoa wa Shinyanga,Kamati za Ulinzi na Usalama pamoja na wachimbaji wa eneo la Mwakitolyo
0 Comments