Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO ASHIRIKI MKUTANO WA KAWAIDA WA 23 WA WAKUU WA NCHI WANACHAMA EAC NGURDOTO ARUSHA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameshiriki Mkutano wa Kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ngurdoto mkoani Arusha Novemba 24, 2023.

Akizungumza mara baada ya mkutano huo Dkt. Jafo amesema kuwa majadiliano yameakisi maeneo muhimu katika sekta ya mazingira hususan mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula.

Amesema Tanzania imekuwa ya mfano barani Afrika kwa kuchukua hatua muhimu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Serikali ya Awamu ya Sita.

Waziri Jafo amesema kuwa kazi kubwa imeonekana kwa upande wa mazingira kwa utekelezaji wa miradi ya mbalimbali ambayo ambayo kwa namna moja ama nyingine inawasaidia wananchi.

“Yamefanyika mapinduzi makubwa kupitia Serikali hususan katika sekta ya kilimo cha kisasa zaidi cha umwagiliaji, mradi wa reli ya kisasa na mabasi ya mwendo kasi yote hii imelenga kupunguza emission,” amesema.

Mkutano huo ulipokea na kuridhia kwa kauli moja mapendekezo ya Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Usalama wa Chakula yaliyofanyika Novemba 23, 2023 ambayo ni hatua ya kuifanya EAC kuwa na msimamo mmoja katika Mkutano wa COP28 utakaofanyika Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia Novemba 28, 2023.

Aidha, mkutano huo umeridhia ombi la Shirikisho la Jamhuri ya Somalia chini ya Rais Mhe. Hassan Sheikh Mahmoud kujiunga na EAC hiyo na kufanya jumla ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa nane.

Mkutano huo umehudhuriwa na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye ambaye amemaliza muda wake wa uenyekiti na kumkabidhi kijiti Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir, Rais wa Kenya Mhe. William Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Rwanda Mhe. Dkt Edouard Ngirente aliyemwakilisha Rais Paul Kagame na Makamu Rais na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasis ya Congo (DRC) aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Antonie Tshisekedi.

Post a Comment

0 Comments