Na Hamida Kamchalla, HANDENI.
WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemtaka Mkurugenzi mkuu wa TANROADS kuharakisha usanifu wa barabara kipande cha km 36 kutoka Mkata hadi kijiji cha Kwamsisi wilayani Handeni ili kuanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa haraka na kuondokana na lawama za wananchi kuhusu mradi huo.
Bashungwa ametoa wito huo katika kijiji cha Kwamsisi wilayani Handeni alipopita kukagua barabara inayotokea Mkata kupitia wilayani Pangani hadi Tanga mjini ambapo alisema tayari fedha za mradi wa ujenzi huo zimeshaingizwa kwa ajili ya matumizi lakini hadi sasa bado hakuna dalili za kuanza kwa ujenzi.
Amesema matamanio ya serikali ni kuona barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kwani maeneo hayo yanazalisha sana hasa zao la muhogo hivyo Rais ametenga fedha ili wananchi wanufaike kwa kutoa mazao yao na kupeleka sokono hasa kipindi cha mvua ambapo magari hayaingii mashambani.
"Na dhamira ya Mh. Rais fedha hazitakiwi zikae benki zinatakiwa ziwe kwenye utekelezaji, kwahiyo hili suala la usanifu wa kina linatakiwa lifanyike mara moja na kwasababu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaitengea fedha na kiu yake kubwa ni kuona barabara hii inajengwa kiwango cha lami",
"Kwahiyo wananchi wa maeneo wa maeneo haya, niwaombe muendelee kumpa ushirikiano Rais wetu, tunaona kwenye mipango yake hajamiacha nyuma na mimi nimekuja kuwasukuma hawa watendaji wetu ili waweze kufanya kazi usiku na mchana kuwatumikia wananchi wetu" amesema.
Waziri Bashungwa amebainisha kwamba mradi huo umechelewa kutokana na michakato mingi ya TANROADS, lakini pia kutojipanga katika utendaji wao kwani tayari kuna baadhi ya maeneo miradi ya aina hiyo imekwishaanza.
"Wananchi hawa, pindi barabara hii itakapokamilika Kwamsisi na maeneo mengine tuliyopita yatabadilika na kupata maendeleo makubwa sana, na hiyo ndiyo ahadi ya chama cha mapinduzi (Ccm),
"Na niwaambie TANROADS muweke jitihada ya kuhakikisha akishapatikana na kumaliza usanifu ndani ya muda, ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami unaanza ili wananchi hawa wapate matunda ya jitihada nzuri za Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan " amebainisha.
Kwa upande wa Mtendaji mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amebainisha kwamba watahakikisha wanafanya jitihada katika utekelezaji na zoezi la usanifu wa kina litakamilika ifikapo mwezi Disemba 31, mwaka huu.
"Mh. Waziri ninaahidi kwamba zoezi la kumpata Msanifu wa barabara hii litakuwa limekamilika tar 31 mwezi Disemba mwaka huu na kazi ya usanifu itaendelea, napenda niwatoe wasiwasi wananchi wa eneo hili kwamba barabara hii mara baada ya kukamika kwa usanifu, tutamtafuta Mkandarasi wa kujenga, kwakuwa fedha zipo" amesema.
Baadhi ya wananchi kijijini hapo wamesema kwa mara ya kwanza tangu walipoambiwa barabara hiyo inajengwa hawajawahi kuona kiongozi kusimama eneo hilo na kuzungumzia maendeleo yake badala yakewanaona magari ya viongozi yakipita tu.
"Leo tumefurahi sana Waziri huyu kusimama na kuongea na sisi kusikiliza kero yetu, shida kubwa hapa ni ubovu wa barabara na hii hali ya mvua, hapa tunalima sana lakini ikifika msimu wa mvua kama hivi mazao yetu yanaozea shambani, hasara tunayopata ni kubwa mno" amesema Fadhil Sefu.
Naye Abdulazizi Bakari amesema, "tulifurahia sana tulipoambiwa barabara hii inawekwa lami lakini sasa tunaona ni ndoto, hasara ni nyingi, hata ukiangalia hali zetu na makazi yetu ni duni, lakini chanzo cha maendeleo kipo na ni hii barabara, ikiwekwa lami hii maendeleo yetu yataonekana, tutajenga nyumba za kisasa tutakapopata masoko ya uhakika kwa kilimo chetu cha mihogo".
0 Comments