Ticker

6/recent/ticker-posts

WASIOKAMILISHA MIRADI YA UJENZI WASIPEWE KAZI--WAZIRI BASHUNGWA.


Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

KUTOKANA na kukwama na kusuasua kwa miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja inayotekelezwa na Makandarasi ambao wanachukua zaidi ya mradi mmoja, Wizara ya Ujenzi inafikiria kuacha kutoa fursa hizo kwa Makandarasi wa aina hiyo.

Akiongea na wananchi wa Wilaya za Handeni na Kilindi katika kijiji cha Mafleta, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameyasema hayo baada ya kukutana na kero nyingi za kutotekelezwa kwa wakati miradi ya ujenzi wa barabara katika Wilaya 3 za Mkoa wa Tanga.


"Sasa nakuagiza Mtendaji mkuu, kama nilivyokueleza kule Kwamsisi, kajipange vizuri kwa hawa Makandarasi ambao siyo wababaishaji ndiyo wapewe kazi na Makandarasi ambao ni wababaishaji wasipewe kazi, muwe na mfumo wakati wa kuanza miradi mipya inaanza kwenye hatua za manunuzi, muwe mnapeana taarifa kama alishaharibu kazi na akiomba asipewe" amesema.


Aidha mradi huo wa barabara ya km 20 unaotokea wilayani Handeni unaishia kijiji cha Mafleta wilayani Kilindi umegarimu kiasi cha sh milioni 30.083 ambazo ni pamoja na fidia za wananchi waliopisha ujenzi wa mradi ulitakiwa kukabidhiwa juni, 6 mwaka huu lakini umeongezewa muda wa miezi 6 na kwamba ulitakiwa kukabidhiwa januari 2024.


"Mkataba huu umeongezwa mara mbili, alitakiwa akabidhi barabara hii mwaka jana mwezi wa 6 akaongezewa tena muda aikabidhi januari 2024, lakini kwa hali ilivyo mpaka sasa hawezi kunidanganya kwamba anaweza akamaliza hii barabara kwa muda mchache huu uliobaki,


"Lakini hapohapo anataka kupewa tena kipande cha km 30 kupitia mfumo wa chanzo kimoja, badala ya kushindanisha na wakati mnajua mvurugo alioufanya, nikwambie Mkurugenzi wa TANROADS, mlikuwa mnafikiria kumuongezea km 30, sasa kwa ugoro huu hakuna kumpa mpaka akamilishe hii km 20" amesema..


Kuhusu fidia za wananchi, Bashungwa aliagiza kwamba, "tuwahudumie watanzania na tutangulize uzalendo mbele sitaki nikirudi mwezi januari nikute ugoro huu nilioukuta hapa leo kabla sijarudi januari wananchi wanaodai fidia wawe wamelipwa, "amesisitiza.


"Dhamira ya serikali kupitia wizara ya ujenzi ni kuona barabara zinajengwa na zinahudumia wananchi wakati uliopangwa kwa mujibu wa mikataba kama kuna wanaotukwamisha wawekwe pembeni tutafute wenye sifa, "amesema Bashungwa.


Akiongelea ujenzi huo kwa niaba ya mbunge wa Kilindi Omari Kibua, Katibu wa mbunge huyo Twaha Mbwego amesema licha ya serikali kumwaga fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini bado tuna kero kubwa ya barabara, kwani kero hiyo inataka kufuta miradi yote mizuri iliyoletwa na serikali.


"Kwa upande wa usafiri hivi sasa nauli kwenye noah tunalipa sh elfu 15 ambayo tulikuwa tunalipa elfu 10, kabla ya barabara kuzidi kuwa mbaya mabasi makubwa yameoandisha nauli kutoka sh elfu 7 mpaka elfu kumi,


"Yote hii inatokana na kero ya ukosefu wa barabara ambayo tayari imeshaanza utekelezaji na kukwama, Mh. Waziri watu wanapoteza maisha njiani wakiwahishwa hospitalini tunaomba muipe uzito barabara hii ya Handeni Kilindi, "amesema.

Post a Comment

0 Comments