Ticker

6/recent/ticker-posts

"WANANCHI MKOA WA MARA KUTOYUMBISHWA NA WAPINZANI, PUNDA HASIFIWI KWA MARINGO BALI MZIGO ALIOUBEBA"


Na, Deborah Munisi


"Kama yupo mtu anayeipinga CCM ni wivu wake binafsi kwasababu katika sekta ya maendeleo inatekeleza kwa kasi, msiyumbishwe na kelele za wapinzani, kufuatia maendeleo haya CCM ina kila sababu ya kutembea kifua mbele"

Ni kauli ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Patrick Chandi wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Nyasho, Musoma Mjini Mkoa wa Mara Novemba 21, 2023 ikiwa ni mwendelezo wa Ziara ya Kamati ya Siasa Mkoa inayoongozwa na mwenyekiti huyo ambaye ameambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara.


Akihutubia wananchi hao amewataka kutoyumbishwa na kelele za wapinzani kwani maendeleo wanayoyaona kwasasa yametokana na msingi bora wa chama tawala wa kuwajali na kuwathamini wananchi wake kwa zaidi ya miaka 60 baada ya ukoloni.


"Punda hasifiwi kwa maringo bali kwa mzigo mzito alioubeba, kwasasa tukiwa na uhitaji wa huduma za afya tunazipata bila tabu yoyote, na hili suala la katiba iliyopo inawazuia kuoa?, msidanganyike hawana jambo zuri la kuwaeleza, Chama tawala kimewahudumia kwa zaidi ya miaka 60 na wakoloni hawakutuachia maendeleo bali maendeleo hayo yamepatikana ndani ya chama Cha Mapinduzi CCM", amesema Chandi

Kwa upande wake Mwita Waitara Mbunge wa Tarime vijijini amewaasa wananchi wa Mkoa huo kuunga viongozi wao mkono ili kukuza maendeleo badala ya kuyadidimiza kwa kutafuta wagombea wao mfukoni na kama ni suala la uchaguzi kila mtu ataonyesha alichokifanya.

"Tunataka siasa tulivu, Hakuna mbunge anayeweza kugawa sukari na matumizi kwenye familia zetu anachokifanya ni kutekeleza majukumu ya kijamii ambayo yanamgusa kila mwananchi na endapo akigundua kuna wagombea wameandaliwa pembeni anaenda Bungeni mwili tu huku akili inabaki jimboni, akirudi anakuja kujibu mapigo na hapo maendeleo lazima mchelewe" ,amesema Mhe. Waitara

Suala la wapinzani nalo akasema “Uchaguzi ujao kila mtu atakula alikopeleka mboga, wameanza kuhaha walianza na bandari, sasa wanaimba katiba, tutakuja na wao watakuja kila mtu aseme na kuonyesha alichofanya, barabara ni mwendo wa kuteleza, kule Tarime kwenda Serengeti, shule za mchepuo wa sayansi nchi nzima, miradi ya kimkakati ya maji mkoani Mara, wapeni salaamu hao watoa taarifa, Mara ni mkoa wa kiumeni, watajua hawajui CCM ndo habari ya mjini,”amesema Waitara.


Naye Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Vedatus Mathayo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani maendeleo Jimboni humo yametekelezwa kwa asilimia mia moja ikiwemo huduma za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara huku utekelezaji wa soko na kusambaza umeme wa REA kwa wananchi wasio na umeme mchakato unaendelea.

"Suala la miundombinu ya barabara hivi karibuni zinatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, na kabla mwezi huu haujaisha mkandarasi anatarajiwa kuingia site kwaajili ya kuingiza umeme wa REA kwa kila mwananchi", amesema Mbunge huyo.

Awali akiwa katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma mjini uliofanyika katika ukumbi CCM Mkoa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma mjini kimemkabidhi cheti Patrick Chandi (MNEC) na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara kwa kuchaguliwa kwa kura za kishindo na kwa kazi nzuri anazoendelea kuzifanya za kuimarisha chama na jumuia zake.


Hata hivyo katika ziara hiyo Chandi amepokea na kusikiliza kero za wananchi na wanachama na kuzitatua na nyingine zikatolewa maelekezo kwa lengo kuzitafutia uvumbuzi, ambapo miongoni mwa kero zao zilikuwa ni Migogoro ya ardhi, Uvuvi haramu, ‘kikokotoo’ kisicho rafiki kwa watumishi, kadi ya bima ya kutodhamiwa, Mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutotibiwa kama Ilani ya CCM inavyoelekeza.

Post a Comment

0 Comments