NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu Cha Dar es Salaam kimejidhatiti kikamilifu kusimamia utekelezaji wa mradi wa mageuzi ya kiuchumi katika elimu ya juu (HEET) ili kuwezesha uboreshwaji wa wa miundombinu ya elimu na hivyo kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuchabgia katika maendeleo endelevu.
Ameyasema hayo leo Novemba 2,2023 Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Maajar wakati wa utiaji saini wa mkataba kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na makampuni mawili yaani M/s Arqes Africa Architects & Interior Designers Limited, na M/s Geometry Consultants Limited kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa majengo takribani 21 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chini ya mradi wa Benki ya Dunia wa HEET.
Amesema kuanza kwa shughuli za ujenzi wa majengo hayo, ni hatua kubwa na mafanikio ya kujivunia katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa elimu ya juu nchini, na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
"Baraza la Chuo limejipanga na linafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu unaopaswa kuleta tija kubwa katika nyanja mbalimbali za taaluma, utafiti na huduma kwa umma hapa chuoni". Amesema
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof.William Anangisye amesema utekelezaji wa Mradi wa HEET umejikita kwenye kuimarisha na kuboresha miundombinu, ikiwemo ukarabati mkubwa na ujenzi wa majengo mapya pamoja na kufunga vifaa vipya kwenye majengo hayo.
Amesema Chuo kinajipanua na kuwafikia watanzania zaidi kwa kuanzisha Kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera katika fani za Kilimo na Biashara.
Aidha amesema kuwa Chuo kimejipanga kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ili kuoboresha ufundishaji na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo ulinzi na usalama.
Nao washauri wa jiometri wa miradi hiyo wameahidi kusimamia weledi na ufanisi ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, kulinda thamani ya pesa iliyitolewa sambamba na kutunza mazingira wakati wa ujenzi wa majengo hayo.
0 Comments