Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania itaendelea kuwalinda watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema hayo wakati akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani leo Novemba 22, 2023 jijini Arusha ambapo amesisitiza Serikali kuendelea kuwa imara katika kuwaepusha na athari hizo.
Dkt. Jafo amesema kuwa watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi hapa nchini na duniani kwa ujumla ikiwemo mafuriko na ukame ambao husababisha baa la njaa.
“Ndugu zangu viongozi Naomba niwathibitishie kuwa dhamira ya Serikali ya Tanzania ni kuwalinda watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi", amesema Waziri Jafo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) nchini Bi. Elke Wisch amepongeza juhudi za Tanzania katika kupigania na kuziendeleza haki za watoto.
Amesema Serikali ya Tanzania imekuwa ikipigania haki za watoto na kuleta maendeleo ambayo matokeo yake yanaonekana katika afya, lishe, ujuzi wa elimu na ulinzi wa mtoto.
Bi. Wisch ameongeza kuwa UNICEF imezingatia maendeleo makubwa yaliyofikiwa kwa watoto na familia zao kote nchini hasa katika kuwalinda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa wito kwa nchi na washirika mbalimbali kuwa pamoja katika kukabiliana na changamoto hizo huku akiitaja Tanzania kama nchi iliyo mstari wa mbele katika mapambano hayo.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba Tanzania iliridhia Mkataba wa Haki za Mtoto mwaka 1991.
0 Comments