Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAJIPANGA KUHAKIKISHA NEMC NA ZEMA ZINAPATA USAJILI GCF

Serikali imejipanga kuhakikisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) zinapata usajili Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (GCF).

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azani Mwinyi aliyeuliza hatua za kusajili taasisi kwenye Mfuko wa GCF.

Amesema kuwa hatua zinazofanyika ni kuwa taasisi mbalimbali zenye nia ya kusajiliwa zinawasilisha maombi katika Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ndiyo mratibu kisha mchakato unaenda GCF inaratibu zikikidhi vigezo zinapata usajili.

Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na mawasiliano, majadiliano na mazungumzo ya kuhakikisha usajili kwa taasisi za Serikali unakamilika.

“Kwa sasa kwa sasa zaidi ya taasisi sita bado hazijafanikiwa kwahiyo tunaendelea kufanya kazi ya kuwahamasisha wenzetu wa Mfuko ili wakubali maombi yetu kwa lengo sasa taasisi zetu ziweze kunufaika,” amesema.

Aidha, Waziri Jafo amefafanua kuwa NEMC tayari imeshaomba na kuanza mchakato wa usajili tangu mwaka 2021 na upande wa ZEMA ilikuwa bado hajawasilisha maombi ya usajili kwenye Mfuko wa GCF.

Hivyo, ameongeza kuwa Serikali itaendeelea kuhakikisha taasisi zote zinazoomba usajili katika Mfuko huo zinafanikiwa kupata usajili ili kunufaika na faida zake.

Katika swali la nyongeza alilouliza kuhusu lini ZEMA wataanza usajili kwenye Mfuko kutokana na uhitaji wa miradi ya mazingira, Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na changamoto ya mazingira Zanzibar, SJMT na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zinashirikiana katika utetekelezaji wa miradi.

Ametaja baadhi ya miradi ni ujenzi wa miundombinu ya kuzuia mawimbi ya bahari kuingia nchi kavu Sipwese Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini – Pemba, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) unaotekelezwa katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini – Pemba.

“Naomba niwahakikishie wabunge kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuhakikisha pande zote mbili za Muungano ziweze kupata fursa hii ya miradi ya maendeleo hususan katika sekta hii ya mazingira,” amesisitiza Dkt. Jafo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azani Mwinyi wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo Novemba 10, 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo (kulia) akifuatilia kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo Novemba 10, 2023.

Post a Comment

0 Comments