Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kuwasilisha taarifa kuhusu utatuzi wa changamoto za Muungano unaofanyika kupitia vikao baina ya Serikali zote mbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Asya Mwadini Mohammed aliyetaka kujua kama kama Serikali haioni haja ya kuwasilisha bungeni taarifa za mchakato mzima wa utatuzi wa changamoto za Muungano.
Akijibu swali hili Waziri Jafo amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikiwasilisha taarifa hiyo katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambayo inaisimamia.
Amesema kuwa hivi karibuni katika vikao vya Kamati za Bunge, miongoni mwa taarifa zilizowasilishwa ni pamoja na ile inayozungumzia Changamoto za Muungano zilizotatuliwa na zile ambazo zinaendelea kutatualiwa ili wananchi wapate ufahamu wa kazi hiyo kubwa inayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
“Nimpongeze mbunge kwa swali lake zuri na tunaahidi kuwa tutaendelea kuleta taarifa za kila tunapotatua changamoto hizi za Muungano katika Bunge lako tukufu Mheshimiwa Naibu Spika hususan katika kipindi cha bajeti na tutaendelea kufanya hivyo kwa vikao vijavyo,“ amesisitiza Dkt. Jafo.
AwaliNaibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu swali la Mbunge wa Konde Mhe. Mohamed issa, amesema mafanikio yaliyotokana na ufumbuzi wa kero 11 za Muungano ni ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Amesema katika maeneo ajira kwa Watumishi wa Zanzibar wanaofanya kazi katika Taasisi za Muungano, wameendelea kunufaika na ajira hizo ikiwa ni asilimia 79 kwa Tanzania Bara na asilimia na 21 kwa Zanzibar.
Amesema Mgawanyo wa Fedha za Mapato yatokanayo na Misaada na Mikopo Nafuu ya Kibajeti (GBS) imeendelea kuongezeka tangu kupatiwa ufumbuzi wa changamoto hii na kuendelea kuimarisha Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa pande zote mbili za Muungano.
Mhe. Khamis amesema tangu kuasisiwa kwa Muungano Serikali zote mbili ziliona ipo haja ya kuunda kamati ya kutatua changamoto katika ngazi mbalimbali.
Amesema kamati hiyo inafanya vizuri ndio maana yamepatikana mafanikio makubwa katika utatuzi wa changamoto za Muungano.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akijibu swali bungeni jijini Dodoma leo Novemba 8, 2023.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu swali bungeni jijini Dodoma leo Novemba 8, 2023.
0 Comments