Ticker

6/recent/ticker-posts

Medea Tanzania Kupitia Mradi wa Jenga Sauti, Kuurejesha Muziki wa Mchiriku

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la MEDEA Tanzania wamekutana na kufanya kikao na wadau wa Sanaa ya Muziki wa Mchiriku kujadili namna ya kuurejesha kwenye fomu baada ya kutamba na kujizoelea umaarufu miaka ya 1990-2000 na kupotea miaka yaa hivi karibuni.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Nov 23,2023, Meneja Ufatiliaji na Tathimini wa MEDEA Tanzania ,Bw.Hassan Kiyungi amesema wameanzisha mradi wa JENGA SAUTI wenye lengo la kuurejesha upya mziki huo ambao kupitia ujumbe wake ulileta ushawishi mkubwa katika jamii katika mambo mbalimbali.

"Miaka ya nyuma muziki wa mchiriku ulikua ukipigwa katika vyombo vya habari na uliweza kuleta ushawishi katika jamii hususani katika ujumbe wake,  miaka ya hivi karibuni ujio wa miziki fulani tena inayofanana na mchiriku umeweza kuathiri muziki wa mchiriku". Amesema

Amesema changamoto inayo ukabili muziki wa mchiriku ni pamoja na jamii kuuchukulia kama muziki wa kihuni,ambapo mara nyingi hupigwa katika maeneo ya uswahilini na mara chache sana kutokea kupigwa katika majukwaa makubwa.

Aidha Bw. Kiyungi amesema katika mradi wao pia wanashughulika kuwapatia mafunzo na kuwajengea uwezo wasanii ili kuzalisha maudhui mazuri ambapo wameanza na bendi mbili Atomic na Jagwa na baadae kuweza kuwafikia makundi ya wasanii wengine.

Pamoja na hayo amesema kuwa wamepanga kuandaa Matamasha kwa ajili ya kuwaweka karibu na hadhira ambao ndio watakuwa wadau wakubwa wa muziki huo ili kuachana na dhana ya zamani kuwa muziki huo ni kwa ajili ya matukio tu kwenye sherehe au harusi.

Kwa upande wake Afisa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bw. Gabriel Awe amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali Sanaa zilizo lala au kuanza kupotea zitaweza kuinuliwa tena na kuweza kufanya vizuri.

Naye Mwanamuziki wa Mchiriku kutoka bendi ya Atomic Bw. Hassan Mtengela ameipongeza Taasisi ya MEDEA kuanzisha Mradi wa JENGA SAUTI kwani unawapatia uwezo na elimu ya mambo mbalimbali ambayo awali hawakuyajua na kubainisha kuwa baadhi ya changamoto zinarekebishika hasa katika upande wa sanaa ya muziki huo.

Aidha Mdau muziki huo na Mtangazaji wa TVE na EFM radio Bw.Fido amesema changamoto mojawapo iliyochangia kukwamisha muziki wa mchiriku ni pamoja na ubabe ambao nyakati zilizopita watu waliogopa kupigwa wale walio kuws wanahudhuria katika maonesho hayo.

"Muziki ili uweze kukua unahitaji kupata mashabiki, labda tu niseme kuwa sahivi muziki mrefu hauna mashabiki kama bolingo,taarabu hata vyombo vya habari huwezi kupiga wimbo wa dakika nane, bado Mtangazaji hajaongea hata sapoti inaweza kugharimu, kwahiyo hili nijambo linalotakiwa kufanyiwa marekebisho" Amesema Bw.Fido.

Post a Comment

0 Comments