Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WATANZANIA wameaswa kumuelewa na kuweka imani zao kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na kauli ya kutaka kuifungua nchi kwakuwa lengo lake ni kuondoa uadui wa kibiashara na kuweka mazingira mazuri na bora ya biashara na uwekezaji nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo lengo la serikali ya awamu ya sita ni kutaka kuona biashara na uwekezaji havipati vikwazo vyovyote hasa katika utekelezaji wake.
"Kazi za msingi za serikali ni kutengeza mazingira mazuri katika biashara, biashara ndiyo huzaa ajira na ajira huzaa fedha hivyo serikali lazima ihakikishe biashara inafanyika, kwahiyo Mh. Rais aliposema anakwenda kufungua nchi alimaanisha anaweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji" amesema.
Aidha amesema kuwa katika upatikanaji wa ajira nchini, kati ya 100 zinazotengenezwa ni ajira 5 tu ndiyo zinatokana na serikali, ajira 95 zinatengenezwa na sekta binafsi kupitia serikali.
"Kwahiyo mtu yeyote ambaye anakwaza sekta binafsi kuwekeza mahali anapotaka, huyo ni adui wa maendeleo ya uchumi na ajira, mara nyingi tumekuwa tunajiuliza kwanini nchi ambazo zimeendelea bado zinapiga hatua na ambazo hazijaendelea zinabaki kuwa masikini".
"Sababu ya msingi kuliko zote ni kwamba nchi zilizoendelea zimejikita zaidi kibiashara na uwekezaji, maadui watatu tangu uhuru ni maradhi, ujinga na umasikini, ni lazima tupambane na tuwashinde hawa maadui watatu" amesisitiza.
Mbali na hayo, Waziri mkuu ametoa maelezo nane kwa Mkoa wa Tanga na Wilaya na halmashauri zake katika suala zima la utendaji kuanzia mamlaka za serikali na kuzitaka kutozuia wawekezaji wala kuwakwamisha kivyovyote.ki
"Mamlaka zote zinazohusika na uwekezaji ziondoe urasimu usio wa lazima kiasi cha kuwakatisha tamaa wawekezaji, mkuu wa Mkoa samaria jambo hili, lakini pia mamlaka zote za serikali za mitaa zitenge maeneo mahususi ya kuyahodhi kwa ajili ya uwekezaji na kuyawekea huduma zote muhimu ikiwemo barabara, wakuu wa Wilaya simamieni hili" ameagiza.
"Mkoa uandae kimkakati wa mawasiliano ili kuongeza kasi ya mawasiliano na kutangaza fursa za miradi zilizopo kwenye maeneo yetu ili ziwafikie wawekezaji wengi zaidi, lakini pia mipango yote ya uwekezaji izingatie maelekezo ya serikali ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira".
Kwa upande wa fursa za uchumi wa bluu Majaliwa alisema, "Mkoa usimamie suala la ulimaji endelevu cha mazao ya bahari, Tanga ina kila aina ya samaki endelezeni kilimo hicho ili kuongeza mazao ya bahari, ili kila mmoja apate kunufaika" amesisitiza Waziri.
Pia ameagiza Mkoa na kuwataka, "wawekezaji wote wa leo na wale mnaotaka kuja mnakaribishwa sana, Tanga ni salama na ushirikiano upo wa kutosha, vilevile kwenu wakuu wa Mikoa fuatilieni kwa karibu utekelezaji wa miongozo ya fursa ya uwekezaji,
"Lakini mwisho, wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, wekeni mikakati ya utekelezaji wa fursa zilizopo katika maeneo yenu kwa kwa kutumia miongozo ya Mikoa sambamba na kubainisha fursa mpya za uwekezaji" amesema.
0 Comments