Ticker

6/recent/ticker-posts

KABURI LAFUKULIWA, MAYAI VIZA, NAZI NA VITAMBAA VYEUSI VYAKUTA NDANI YAKE, USHIRIKINA WAHUSISHWA


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MWANAMKE mwenye asili ya Kiarabu anayedaiwa kuuwawa na watu wasiojulikana na kuzikwa kwenye eneo la Mwekezaji eneo mtaa wa Mafuriko, kata ya Mzizima, jijini Tanga limefukuliwa na serikali.

Baada ya kufukuliwa kaburi hilo mwili wa marehemu haukuwepo bali kulikutwa mayai viza, nazi pamoja na vitambaa vyeusi hali iliyoleta taharuki kwa wananchi wa mtaa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, James Kaji amefika eneo hilo amrsema mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi walichukua hatua za kulifukua kwa kibali cha Mahakama ambapo baada ya kufukua kaburi wamekuta mambo ya imani za kishirikina ikiwemo kukutana na sanda nyeusi, nazi tatu na yai viza.

“Ni kaburi ambalo lilionekana lipo ndani ya eneo la Mwekezaji lakini sambamba na hilo wakati tunaendela na ufukuaji tumekuta wananchi wengi wamevamia eneo hilo ambalo limepimwa viwanja kwa kisingizio kwamba hawana maeneo ni kana kwamba wametengeneza tukio hilo ili kumtisha Mwekezaji na watu waliopimiwa viwanja” amesema.

Aidha Kaji amepiga marufuku ya kutoonekana kwa mtu yeyote katika eneo hilo na kusema kuwa kumekuwa na tabia ya wananchi kuvamia maeneo ya wazi na baadaye kuomba fidia kwa serikali.

Hata hivyo amebainisha kwamba wananchi wamezoea kujichukulia maeneo na kuweka makazi ya kudumu na inapotokea serikali inayahitaji wanakimbilia kwa wanasiasa kupata msaada jambo ambalo wanasiasa hao wanapata mianya ya kutanguliza kivuli cha wapiga kura.

"Tabia hii haipendezi kabisa na imekuwa ikiiletea serikali matatizo makubwa ya migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi ni uvamizi wa wananchi kwenye maeneo yenye hati miliki,

“Nimetoa onyo na hatutamvumilia mtu yeyote na wengi wamekuwa wakikimbilia kwa wanasiasa kwamba ni wapiga kura wetu hilo halitakuwepo na hatutalivumilia, Tanga tunaweza kuishi bila migogoro ya ardhi" amesema Kaji.

Baadhi ya wananchi wameeleza kwamba tukio la kuzikwa mwanamke huyo lilifanyika lakini cha kushangaza ni kutoona dalili zozote zinazoonesha kama alizikwa hapo na kwamba bado hawaamini kwa kilichotolewa ndani ya kaburi hilo.

"Cha kushangaza ni kwamba, watu waliamini kwamba marehemu alizikwa kaburini humo, sasa hivi vitu vilivyotolewa hapa siyo vya kawaida kabisa, imani iliyojengeka ni kuhusu ushirikina jambo ambalo kwakweli limetuletea taharuki na hofu" amesema Yusuf Mwinjuma.

Post a Comment

0 Comments