Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ameongoza ujumbe wa Wajumbe wa Bodi kutoka Afrika wa Shirika la Kimataifa la Lishe (Nutrition International, NI) kukutana na Spika wa Bunge la Kanada Gregory Fergus katika Ofisi za Bunge la nchi hiyo zilizopo Ottawa, Kanada. Kikao hicho kimehudhuriwa pia wajumbe wengine wa Bodi hiyo ambao ni Dkt. Ibrahim Mayaki, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger na Bi. Vivian Onano kutoka Kenya.
Dkt. Kikwete na ujumbe alioambata nao walitumia fursa ya kikao hicho kueleza kwa undani kazi kubwa zinazofanywa na Shirika hilo la Kimataifa la Lishe lenye makao makuu nchini Kanada katika kupambana na tatizo la utapiamlo duniani, hususan katika nchi zinazoendelea zikiwemo za bara la Afrika.
Spika wa Bunge la Kanada, Gregory Fergus akisisitiza jambo katika kikao hicho
Aidha, kupitia kikao hicho kilichohudhuriwa pia na wajumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge hilo, Dkt. Kikwete aliishukuru Kanada kwa kuendelea kufadhili kazi za Shirika hilo la NI kwa zaidi ya miaka 30 ambapo kupitia kazi zake takriban maisha milioni 34 ya watoto wachanga, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wasichana balehe na wanawake wajawazito yameokolewa duniani kote, hususan katika nchi za bara la Asia na Afrika.
Kwa upande wake Spika Fergus alimshukuru Dkt. Kikwete na ujumbe alioambatana nao kwa kutambua umuhimu wa kulishirikisha Bunge la Kanada katika kazi kubwa inayofanywa na Shirika hilo lisilo la kiserikali. Akamweleza anatambua kuwa lishe bora ni moja ya haki za msingi za kila mwanadamu na kwamba Kanada itaendelea kuwa nchi kinara katika kufadhili miradi mbalimbali inayolenga kuboresha upatikanaji wa lishe bora na virutubisho duniani.
Mbunge wa Kiliberali wa Bunge la Kanada, Arielle Kayabaga, ambaye ni mzaliwa wa Burundi akichangia katika Kikao hicho
Shirika hilo lenye Ofisi katika nchi tano za Afrika zikiwemo Tanzania, Ethiopia, Kenya, Nigeria na Senegal limejikita katika kutoa lishe nyongeza zilizothibitishwa kitaalamu, zenye ufanisi wa hali ya juu na zinazopatikana kwa gharama nafuu. Kupitia programu kama vile urutubishaji wa nafaka na mafuta ya kula, na uwekaji wa madini ya joto kwenye chumvi (iodini), Shirika hilo la la NI linasaidia jitihada za Serikali za nchi zinazoendelea kukabiliana na tatizo la udumavu na unyafuzi kwa watoto, yaani watoto kuwa na urefu au uzito mdogo zaidi kulingana na umri wao.
Udumavu na unyafuzi bado ni tatizo kubwa duniani ambapo tathmini ya hali ya utapiamlo duniani ya mwaka 2023 iliyofanywa kwa pamoja Shirika la Afya Duniani (WHO), Mfuko wa Kimataifa wa Watoto (UNICEF) na Benki ya Dunia (WB) inaonesha kuwa angalau mtoto mmoja kati ya watano wenye umri chini ya miaka mitano (takribani watoto milioni 148.1) ana udumavu na wengine milioni 45 wana unyafuzi. Nchi zinazoendelea zinakabiliwa zaidi na tatizo hili.
Picha ya pamoja: Kutoka kushoto ni Bw. Joel Spicer, Rais na Mtendaji Mkuu wa NI, Bi. Arielle Kayabaga, Mbunge, Bi. Vivian Onano, Mjumbe wa Bodi ya NI kutoka Kenya, Spika Gregory Fergus, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Bw. Mike Lake, Mbunge, Dkt. Ibrahim Mayaki, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger na Mjumbe wa Bodi, Bi. Salma Zahid, Mbunge na Bw. David de Ferranti, Mwenyekiti wa Bodi ya NI.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini Tanzania ya 2022 iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaonesha kuwa tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano bado ni kubwa hapa nchini. Ripoti hiyo inaonesha kuwa 30% ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 hapa nchini wana udumavu huku 3% wakiwa na unyafuzi.
Aidha, ripoti imeainisha kuwa watoto wa umri huo hapa nchini pia wanakabiliwa na changamoto nyingine za utapiamlo ambapo takriban 12% wana uzito ulio chini ya kiwango (underweight) na 4% wana uzito uliozidi kiwango (overweight). Shirika la NI ni mmoja wa wadau walioshirikiana na Serikali katika kuandaa Ripoti hiyo.
Spika Fergus akifurahia jambo la Rais Mstaafu Kikwete wakati akimwonesha baadhi ya Hansard za Bunge hilo lililoanzishwa mwaka 1867.
Wataalamu wa afya wanaeleza kwamba endapo utapiamlo hautodhibitiwa katika siku 1000 za awali za mtoto basi madhara yake yanaweza kuwa ya kudumu yasiyoweza kurekebishika. Pamoja na mambo mengine, hii hupelekea mtoto kudumaa kiakili na kimwili na hivyo kupata ugumu wa kufundishika na kuelewa masomo na kuwa na utambuzi hafifu. Aidha, magonjwa yanayotokana na utapiamlo kama vile upungufu wa damu, upungufu wa wekundu wa damu, ukosefu wa vitamini C, vitamini A na madini joto ni moja ya chanzo kikubwa cha vifo vya watoto na wanawake wanaojifungua.
0 Comments