Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mtatiro Kitinkwi,akiongea wakati wa uzinduzi huo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe (kushoto) akibadilishana mawazo na Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa mkoa wa Polisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi (katikati) na Afisa Uhusiano wa Barrick nchini, Georgia Mutagahywa, wakati wa hafla ya uzinduzi huo.
Baadhi wa Maofisa wa Jeshi la Polisi wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Burudani za ngoma kutoka vikundi vya utamaduni vya Jeshi la Polisi pia zilikuwepo.
Wanafunzi wa shule pia walihudhuria katika maadhimisho hayo
*
Kampuni ya Barrick nchini, imeahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini na wadau mbalimbali katika kuelimisha jamii kutojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Haya yamebainishwa wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, yaliyofanyika katika viwanja vya kituo cha Polisi cha Mango Garden , Kinondoni, ambapo Mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe.
Maadhimisho haya yaliambatana na kutoa mafunzo kuhusuana na vitendo vya ukatili wa kijinsia yaliyoendeshwa na Maofisa Waandamizi na wataalamu wa masuala ya jinsia na sheria kutoka Jeshi la Polisi wanaosimamia madawati ya kijinsia.
Akiongea katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na askari kutoka vikosi mbalimbali, wanafunzi, Wananchi, Meneja Uhusiano wa Barrick, Georgia Mutagahywa, alisema, kampuni hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali wanaotoa elimu ya ukiukaji wa haki za Binadamu ikiwemo ukatili wa kijinsia na ndio maana kwa mara nyingine mwaka huu imeamua kushirikiana na Jeshi la Polisi kufikisha elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii katika wilaya zote za Dar es Salaam na mikoa mingine.
“Katika siku hizi 16 za maadhimisho haya tumejipanga kwa kushirikiana na madawati ya Kijinsia ya Jeshi la Polisi kufikisha elimu hii mashuleni ikiwemo sehemu mbalimbali za jamii na siku zote tutakuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo katika mapambano haya",alisema.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stela Msofe, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, alisema kama wanayobainisha wataalamu wa masuala ya jinsia, jamii inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukatili wa kimwili, ukatili wa kihisia pamoja na ukatili wa kiuchumi hivyo sio kazi ya Jeshi la Polisi tu kupambana na changamoto hii bali ni kujumu la kila mmoja kupaza sauti.
Aliwataka wananchi wote kuungana kupaza sauti wakati wote dhidi ya vitendo vya ukatili wa jinsia sambamba na kutoa elimu katika jamii, vilevile aliwapongeza wanaharakati na wadau mbalimbali ambao wanaunga mkono Jitohada za Serikali katika mapambano haya wakati wote.
“Kama ilivyo kauli Mbiu ya Maadhimisho haya mwaka huu isemayo Wekeza Kuzuia Ukatili wa Kijinsia, natoa wito kwa kila mmoja wetu kutofumbia vitendo hivi maana vipo na vinaendelea na kundi kubwa linaloathirika ni watoto hivyo wazazi tunao wajibu mkubwa kuhakikisha tunakilinda kizazi hiki”,alisema Msofe.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mtatiro Kitinkwi, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kuhakikisha linawafikisha kwenye vyombo vya sheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivi.
Afande Kitinkwi, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kutoa taarifa kwenye madawati ya jinsia ambayo yameanzishwa kwa ajili ya kushughulikia changamoto za matukio yanayohusiana na kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia huanza kila ifikapo Novemba 25 na kufikia kilele Desemba 10 ya kila mwaka ikiwa na lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili kwa jamii. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia”.
0 Comments