Ticker

6/recent/ticker-posts

JENGENI TABIA YA UKAGUZI WA BARABARA MTABAINI CHANGAMOTO KABLA YA ATHARI - BASHUNGWA.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MAMENEJA wa TANROADS nchini wameelekezwa kuweka utaratibu wa kukagua mitandao ya barabara iliyoko ndani ya Mikoa yao ili kubaini matatizo kabla hakujatokea madhara yanayopelekea hasara kubwa kwa serikali pamoja na wananchi.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alipopita kuangalia darala la Bwiko lililopo mpakani mwa Mikoa ya Tanga na Kilimanjaro ambalo wakati huu mvua zibazoendelea kunyesha lilijaa maji na kukatika.

Bashungwa amesema barabara ya kuanzia Chalinze Mkoa wa Pwani kuelekea Tanga hadi Kilimanjaro na Arusha ni kati ya zilizoathirika na zina mashimo mengi huku akisisitiza Mameneja wa Mikoa hiyo kuangalia namna ya kufanya ukarabati wa dharura.

"Mkae muangalie bajeti zenu na muungane kwa pamoja ni lazima barabara hii itengenezwe na ifanyiwe ukarabati, mahali ambapo mabega yamechoka yarudishwe kwenye ubora wake, maeneo ambayo madaraja yanafanana kama hapa tulipo mchukue tahadhari mapema",

"Lakini niwapongeze kwa namna ambavyo mmepawahi hapa kwa kuchukua hatua za haraka, Mtendaji mkuu na timu yako, ukisaidiwa vema na Meneja wa Mkoa na timu yake, nikupongeze sana meneja, hivi ndivyo inavyotakiwa kufanya inapotokea dharura" amesema.

Aidha Bashungwa amewataka baadhi ya wananchi kuacha mara moja tabia ya kufanya upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii kwa kupiga picha maeneo ambayo yamepata athari ya mvua na kutupia mitandaoni wakitangaza hali ya hatari ma mafuriko.

"Unaweza ukute picha inazunguka mitaoni jambo lenyewe limetokea mwaka jana mtu anakuja kuliweka leo kwa makusudi kuleta taharuki kwa wananchi pasipo na sababu, kana kwamba hilo jambo limetokea sasa hivi, hii siyo tabia nzuri na niwaombe Watanzania tuendelee kukemea tabia ya watu hawa ambao siyo waungwana" mesisitiza.

"Lakini pia niwashukuru wananchi ambao wanaendelea kutupatia, nimekuwa nikipokea sms mbalimbali kuhusu maeneo ya barabara ambayo yanahitaji sisi kuingilia kati, huo ni ushirikiano mzuri ambao naupongeza kutoka kwa wananchi na pia wawe sehemu ya kukemea wale wachache wenye tabia ya kuharibu miundombinu. amepongeza.

Hata hivyo amewasihi wananchi juu ya utupaji wa taka hovyo kwenye maeneo ya mifereji ya maji na kusisitiza kwamba suala hilo ni kwa barabara zote nchini iwe ya TANROADS au ya TARURA ili kuepusha uchafuzi wa mazingira ikiwe mifereji au madaraja kuhaa uchafu.

Mbali na hayo Waziri Bashungwa amebainisha kwamba kupitia ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Tanga ataendelea kuwapima watendaji hao kwa maagizo aliyowapa kuyafanyia kazi.


Naye Mtendaji mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema wamepokea maelekezo yote ya Waziri na kwamba kupitia maagizo hayo uwezekano wa kuimarisha Taasisi hiyo kwa haraka ni mkubwa na tayari wamejipanga kwa hilo.


"Taasisi imejipanga kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha kuwa barabara zao zinadumu na kumaliza tatizo la kuharibika kabla ya wakati uliopangwa ikiwa ni pamoja na kuwapa kazi Makandarasi ambao hawana uwezo,


"Jinsi ya kudhibiti hali ya barabara ni kuhakikisha tunasimamia kikamilifu utekelezaji na usimamizi mzuri unakuja tu pale ambapo wataalamu katika taasisi wanajengwa na kuinuliwa, lakini pia kwenye suala la usanifu, tutafanya usanifu uwe wa kina zaidi ili kuhakikisha tunaondoa kabisa mazingira ambayo yanaweza yakaleta athari" amebainisha.

Post a Comment

0 Comments