Ticker

6/recent/ticker-posts

BoT YAWAASA WANANCHI KUEPUKA MIKOPO UMIZA


**************

WAKOPAJI katika benki na taasisi za fedha wametakiwa kuzingatia mambo muhimu kabla ya kuchukua mkopo ili kujiepusha na changamoto wakati wa kurejesha fedha hizo.

Hayo yameelezwa na Afisa Mkuu Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania Bwana Deogratias Mnyamani, katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha ambapo amesema kwanza mkopaji anapaswa kuelewa vigezo na masharti yaliyopo katika mkataba wake.

Pia, mkopaji anatakiwa kuchukua nakala ya mkataba wa mkopo, ili wakati atakapopatwa na changamoto aweze kusaidika kwa wepesi.

Mnyamani amesisitiza kuwa wateja wanapaswa kukopa na kuweka akiba zao katika sehemu rasmi kama Benki, SACCOS na vikundi vilivyosajiliwa kwani vyote hivi vipo chini ya Wizara ya Fedha na kwa kufanya hivyo mteja atakuwa sehemu salama yeye pamoja na fedha zake.

Amesema pia wakopaji wanapaswa kuelekeza fedha wanazochukua katika mambo ya msingi,ambayo yatawaletea faida na kuwawezesha wao binafsi kurejesha fedha hizo.

"Tafiti ndogo tuliyoifanya inaonyesha watu wanachukua mikopo na kuelekeza katika maeneo ambayo sio stahiki, kama katika sherehe za harusi, kumbukumbu za kuzaliwa na kushona sare katika sherehe tofauti tofauti"

"Kwa kuelekeza fedha za mkopo katika mambo kama hayo, mkopaji hatoweza kurejesha kwani hazalishi bali ameteketeza na hapo ndipo anapoingia katika changamoto katika urejeshaji" amesema Mnyamani.

Mnyamani ameeleza kuwa kwa upande wa taasisi za fedha pamoja na Benki wanapaswa kuwapa wateja uwanja wa uwezekano wa kuendelea kulipa mkopo pale ambapo mteja amepata changamoto ya kulipa mkopo huo, mradi tu mteja anaendelea kulipa hata kama uwezo wake umepungua.

Ameeleza kuwa taasisi za fedha na benki zinapaswa kutoa muda wa urekebishaji kwa wateja wao na kutoa elimu ili kuwasaidia watu wengi kujiepusha na changamoto wanazokabiliana nazo kwa kutokujua masharti ya mikataba wanayoingia.

Kauli mbiu ya wiki ya fedha kwa mwaka 2023 ni "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya kiuchumi" ambapo Benki Kuu ya Tanzania inashiriki katika maadhimisho hayo kwa kutoa elimu ya fedha kwa umma ikiwa ni pamoja na elimu mahususi itakayo wasaidia watu kujua nini wanapaswa kufanya kabla ya kuchukua mkopo.

Maadhimisho ya wiki ya fedha yamefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha kuanzia tarehe 20 hadi 26 Novemba 2023

Post a Comment

0 Comments