Na Mwandishi Wetu Iringa.
Watumishi zaidi ya 603 kutoka Wizara, Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali wanaoshiriki mashindano ya 37 ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mkoani Iringa wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha lengo likiwa ni kujionea vivutio vya Utalii vilivyopo katika Hifadhi hiyo.
Hatua hiyo inakuja kufuatia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Taasisi zake katika kutumia kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Timu ya Wizara , Bi. Getrude Kassara amesema wametumia fursa ya michezo ya SHIMIWI kuhamasisha utalii wa ndani suala ambalo limeleta matokeo chanya kwa watumishi hao kutembelea Hifadhi hiyo.
"Tumeona tutumie fursa hii kuweza kuhamasisha watumishi wenzetu ambao pengine hawajui kama fursa hii ipo katika maeneo haya ili wakitoka huku wakawe mabalozi wa utalii katika familia zao na Taifa kwa ujumla", amesema Bi. Kassara.
Aidha, ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara kwenye kuhamasisha na kuutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini Duniani kote
"Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani yeye amekuwa kinara wa kuhamasisha na kutangaza utalii Duniani kote na Muongoza watalii namba moja hivyo na sisi Watumishi tumehamasika kwa kutembelea vivutio hivi vya utalii", amesema Bi. Kassara.
Vilevile, Bi. Kassara amechukua fursa hiyo kupongeza Mradi wa REGROW kwa kununua magari ya kuboresha na kutangaza Utalii. Pia, kwa kuendelea na jitihada zake za kuutangaza utalii wa nyanda za juu kusini huku akisisitiza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ina vivutio vya kipekee ukilinganisha na vivutio vingine hapa nchini
Kwa upande wake Mchezaji kutoka Wizara ya Nishati, Bi. Zaituni Issa amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza mengi na ametumia fursa hiyo kuwahimiza Watanzania kutembelea vivutio mbaalimbali vilivyopo hapa nchini
Kwa upande wake mchezaji wa Riadha kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Elibariki Buko amesema ziara hiyo inatoa fursa ya kujifunza nakujionea vivutio mbalimbali vilivyopo kwenye hifadhi hiyo.
"Tumeona wanyama mbalimbali katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Tumeona Tembo, Tumeona Twiga, Swala, Mito, Mamba na vivutio vingi vinavyopatikana ndani ya Hifadhi hii", amesema Buko.
Katika hatua nyingine, Buko ametoa wito kwa Watanzania wote kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha waliyotemblea leo pamoja na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii hapa nchini.
0 Comments