Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKILI AIPIGA JEKI SEKONDARI YA MUHWANA, IRINGA VIJIJINI

Mwandishi Wetu, Iringa

SHULE ya Sekondari ya Muhwana iliyoko katika kijiji cha Magulilwa wilayani Iringa, imepata msaada wa kompyuta na mashine ya kudurufu mitihani na nyaraka zake zingine ili kuiongezea ufanisi katika utoaji kwa wakati huduma zinazohitaji vifaa hivyo.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 6.5 umetolewa na mdau wa maendeleo wa wilaya hiyo, Sosten Mbedule ambaye ni wakili wa kujitegemea.

Kupatikana kwa mashine hizo kunamaliza changamoto ya ukosefu wa huduma ya kudurufu mitihani na nyaraka nyingine iliyokosekana katika shule hiyo kwa miaka mingi.

Akikabidhi msaada huo wakati shule hiyo ikifanya mahafali yake ya 14 ya kidato cha nne, Mbedule alisema; "Niliitikia ombi la shule la kusaidia kupatikana kwa vifaa hivi kwa kuwa mimi ni mdau wa maendeleo lakini pia ni zao la shule za kata."

Jumla ya wanafunzi 138 kati ya 234 walioandikishwa kidato cha kwanza wamehitimu kidato cha nne huku waliobakia wakishindwa kukamilisha ndoto zao za kupata kiwango hicho cha elimu kwasababu mbalimbali ikiwemo mimba na utoro.

Akipongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia wakili huyo alisema kuinga mkono serikali katika kuboresha elimu ni hatua muhimu na inaweza kuchangia maendeleo bora ya nchi.

"Kuchangia vifaa vya shule, vitabu, na vifaa vingine vya kujifunzia kunaweza kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia. Kazi hii haiwezi kufanywa na serikali pekee ni muhimu wadau wengine tukachangia," alisema.

Aidha Mbedule amesikitishwa na taarifa ya idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo kushindwa kumaliza kidato cha nne akisema kutatua tatizo hilo jitihada za pamoja kati ya serikali, jamii, na wadau wa elimu zinahitajika.

Mbedula alisema hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika elimu, kuboresha upatikanaji wa rasilimali, kutoa msaada kwa wanafunzi masikini, na kuendesha programu za kuhamasisha wanafunzi kuendelea na masomo yao.

Aliwata wanafunzi wanaokaribia kufanya mitihani yao ya kidato cha nne kuunda umoja wa kusoma, kukumbushana na kusaidiana kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha kila mmoja anapata matokeo mazuri.

Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Donald Kilundo amemshukuru Wakili Mbedule kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo shuleni hapo huku akiutaja mchango wake shuleni hapo unavyosaidia kutatua changamoto za kielimu shuleni hapo.

Hata hivyo Kilundo alisema shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto za miundombinu hasa ukosefu wa hosteli za wanafunzi wa kike na kiume jambo linalopelekea utoro na mimba kwa wanafunzi na kuomba wadau kuendelea kusaidia kutatua changamoto hizo.

Kilundo alisema changamoto hiyo inawakosesha wanafunzi utulivu wa mazingira ya kujifunzia huku wengi wakipanga nyumba mtaani.

Post a Comment

0 Comments