Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKAZI WA MAGU WAASWA KUENDELEA KUCHANGIA DAMU KUOKOA MAISHA

Wananchi wa Wilaya ya Magu wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania wanaohitaji damu ili kusaidia uwepo wa damu ya kutosha na kuweza kusaidia maisha ya wagonjwa .

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu Bi. Rachel Kassanda wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo aliongoza Wananchi katika zoezi la uchangiaji damu na kutoa misaada mbalimbali katika hospitali ya Wilaya ya Magu kama sehemu ya kumbukumbu ya kuyaenzi maono ya Mwalimu Nyerere.

" Nawaomba wananchi wa Magu wajitolee kuchangia damu ukiona afya yako ni nzuri na una uwezo njoo uchangie ili uokoe maisha ya mtanzania mwenzako mwenye uhitaji ambae angeweza kupoteza maisha kwa kukosa damu yako " amesema DC Kassanda

Amesema Wilaya ya Magu imeadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa kwa kuwajulia hali wagonjwa na kutoa misaada mbalimbali katika hospitali ya Wilaya ya Magu kama ishara ya kuyaenzi maono ya Baba wa Taifa.

" Mh Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Mwakilishi wake Mkuu wa Wilaya ya Magu tumemkumbuka Baba wa Taifa kwa kuwatembelea wagonjwa na kutoa misaada mbalimbali kwa wahitaji waliopo katika wodi mbalimbali Hospitali hapa"

Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa waendesha bodaboda Wilaya ya Magu , Mohamed Jumanne amesema wameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkuu wa Wilaya ya Magu kuadhimisha kumbukizi ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa kwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto na kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu.

Aidha Mwenyekiti huyo amewahamasisha vijana mbalimbali waliopo Wilaya ya Magu kuendelea kujitokeza kuchangia damu katika hopsitali zilizopo Wilaya ya Magu .

Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda ( kulia ) akiongozana na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Jubilete Lauwo ( katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bi Fidelica G. Myovella ( kushoto) kuelekea wodi ya wazazi kwaajili ya kutoa msaada ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda akifikisha salamu za Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa kinamama katika wodi ya watoto Hospitali ya Wilaya hiyo mara baada ya kutoa misaada mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba 14, 2023.
Baadhi ya madereva bodaboda waliojitokeza kuchangia damu wakiendelea na zoezi la uchangiaji damu katika Hospitali ya Wilaya ya Magu  ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba 14, 2023.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda akimsalimia mama na mtoto katika wodi ya wazazi baada ya kumkabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Post a Comment

0 Comments