Timu ya mpira wa miguu pamoja na mpira wa pete za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) zimefanikiwa kufuzu katika hatua ya 16 bora katika Michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea Mkoani Iringa.
Katika Michuano hiyo timu ya mpira wa miguu imemaliza mzunguko wa hatua ya makundi pasipo kupoteza mchezo wowote ikiongoza kundi C kwa jumla ya point 10 kati ya michezo 4 iliyocheza huku timu ya mpira wa pete ikipoteza mchezo mmoja pekee.
Akizungumza mara baada ya ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya timu ya Mashtaka, Kocha wa timu ya mpira wa miguu ya OSHA, Bw. Bashiru Daima amesema kuwa siri kubwa ya mafanikio hayo ni nidhamu iliyooneshwa na wachezaji wake katika kipindi chote cha maandalizi pamoja na morali ya wachezaji wake katika michezo yote waliocheza.
“Katika Michezo yote minne ya mzunguko wa hatua ya makundi tunashukuru Mungu hatujapoteza mchezo wowote na tumemaliza tukiongoza kundi C kwa jumla ya Point 10, hii yote ni kutokana na morali ya wachezaji wangu ya kuutaka ushindi katika kila mechi ndio maana wamepambana kwa nguvu zote hadi kufikia hatua hii na tunaamini tutafanya vizuri katika hatua zingine kwasababu wachezaji wako imara na hakuna majeruhi hadi sasa.” Alisema Bw. Bashiru Daima.
Aidha nahodha wa timu ya mpira wa miguu, Bw. Joseph Mbunda amesema kuwa katika Michuano hii ya 37 timu ya soka imekuwa na kikosi bora sana kwasababu wamekuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi na kuelewa vyema mbinu mbalimbali za kuwakabili wapinzani walizofundishwa na mwalimu wa kikosi hicho.
“Tumekuwa na muda mrefu sana wa kufanya maandalizi kwajili ya michuano hii na pia tumekuwa tukimsikiliza vizuri sana mwalimu wetu hii imetujengea kikosi bora sana na ari ya kushinda dhidi ya wapinzani wetu tunaokutana nao, tunaahidi ushindi katika hatua zijazo” alisema Joseph Mbunda.
Kwa upande wake nahodha wa Timu ya Mpira wa Pete,Bi. Rachel Nkoma amesema kuwa wachezaji wake wamejipanga ipasavyo kukabiliana na wapinzani katika hatu zinazofuata huku akiahidi kufanya vuziri zaidi katika Michuano hii ya 37 kutokana na maandalizi makubwa yaliyofanyika kabla ya michuano hii kuanza.
Nae katibu wa Michezo wa OSHA, Bw. Ally Mwege amesema kuwa katika kipindi chote cha maandalizi ya michuano hii uongozi ulijenga umoja na nidhamu kubwa kwa wanamichezo wote huku akimshukuru Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda kwa kuiwezesha timu katika mahitaji mbalimbali ikiwemo vifaa vya michezo
“Tulipofika Mkoani Iringa kwajili ya michuano hii uongozi ulihakikisha wachezaji wote wanakaa kwenye kambi na wanazingatia masharti yote ya kambi vilevile tunapenda kuushukuru uongozi wa OSHA Chini ya Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda kwa kutupatia mahijati muhimu katika kipindi chote cha maandalizi ikiwemo vifaa vya michezo , waalimu wa timu zetu, wataalamu wa huduma ya kwanza ili kutoa huduma pindi wachezaji wanapopatwa na changamoto za kiafya,usafiri uliyotuwezesha kufika huku n.k.
Timu ya mpira wa miguu ya OSHA inatarajia kucheza mchezo wake wa hatua ya 16 bora dhidi ya timu ya TAKUKURU tarehe 6/9/2023 huku timu ya mpira wa pete ikicheza mchezo wake dhidi ya Bohari ya Dawa (MDS).
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Mhe. Dkt. Dotto Biteko akikabidhi mpira kwa manahodha wa timu za OSHA na HAZINA wakati wa mchezo wa ufunguzi wa Michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambapo timu hizo zilicheza mchezo wa ufunguzi.
Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya OSHA wakiwa katika picha ya Pamoja kabla ya kucheza mchazo wao wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo mchezo ulimalizika kwa sare ya kufungana bao moja kwa moja.
Wachezaji wa timu ya mpira wa pete na mpira wa miguu wa OSHA wakifurahia ushindi wa bao 30:4 dhidi ya timu ya Tume ya Utumishi.
Kikosi cha timu ya mpira wa pete cha OSHA kikiwa katika picha ya Pamoja kabla ya mchezo wake dhidi ya HAZINA uliokuwa ni miongoni mwa mechi za ufunguzi wa mashindano ya SHIMIWI katika dimba la Samora Mkoani Iringa
0 Comments