Ticker

6/recent/ticker-posts

Tanzania na Uganda wajadiliana Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia

--  Rasimu ya Mkataba baina ya nchi hizo mbili kusainiwa mwezi Novemba, 2023

Serikali ya Tanzania na Uganda zimekubaliana kuwa Rasimu ya Mkataba Mahsusi Baina ya Tanzania na Uganda (Bilateral Agreement) katika utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda isainiwe Mwezi Novemba, 2023 Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga na Naibu Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Peter Lokeris wamekubaliana hayo wakati wa kikao cha majadiliano kuhusu Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Uganda kilichofanyika terehe 26 Oktoba 2023, Jijini Dar es salaam.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Musa Makame na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Nishati upande wa Tanzania na Uganda.

Akizungumzia hatua zilizofikiwa katika majadiliano hayo, Mhe. Kapinga alisema kuwa Wizara ya Nishati, imekwisha wasilisha nyaraka muhimu kwa wadau wote wanaohusika katika utekelezaji wa mradi huo ikiwemo Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Pia Wizara imeshapokea maoni kutoka kwa wadau hao, ambapo tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameridhia kuendelea na hatua zinazofuata.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Peter Lukeris amesema kuwa mradi huo ni muhimu kwa nchi zote mbili hivyo ni vyema kuanza utekelezaji wa hatua za awali hususani kusaini nyaraka zilizoandaliwa ikiwemo Rasimu ya Mkataba Mahsusi Baina ya Tanzania na Uganda (Bilateral Agreement).

Vilevile ameeleza kuwa kusainiwa kwa mkataba huo utawezesha shughuli zingine za utekelezaji wa mradi huo kuanza na kuleta manufaa kwa mataifa hayo mawili.

Awali akiwasilisha taarifa za mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Mramba, alieleza kuwa Timu ya Wataalamu ya pamoja iliandaa nyaraka mbalimbali ambazo ni Rasimu ya Mkataba Mahsusi Baina ya Tanzania na Uganda (Bilateral Agreement), Rasimu ya Kanuni za Manunuzi za Pamoja (Joint Procurement Rules) na Rasimu ya Hadidu za Rejea (Terms of Reference - ToR).

Na baada ya kuandaa nyaraka hizo, timu hiyo ya watalaam ilikubaliana kupata maoni na idhini kutoka Mamlaka zinazohusika na Mradi huo kutoka nchi zote mbili na kuzifanyia kazi kwa hatua zaidi.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (katikati), Naibu Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Peter Lokeris (kulia) na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao kuhusu utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Uganda kilichofanyika terehe 26 Oktoba 2023, Jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Peter Lokeris (katikati) na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (wa tatu kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Uganda, kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Musa Makame, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, baada kikao kuhusu utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Uganda kilichofanyika terehe 26 Oktoba 2023, Jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (kushoto) na Naibu Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Peter Lokeris (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja baada kikao kuhusu utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Uganda kilichofanyika terehe 26 Oktoba 2023, Jijini Dar es salaam.

Post a Comment

0 Comments