Dar es Salaam tarehe 21 Oktoba 2023
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa kufanyika tarehe 24 Oktoba 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia amealikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mheshimiwa Hakainde Hichilema.
Mheshimiwa Dkt. Samia pia amealikwa kufanya Ziara ya Kitaifa nchini Zambia kuanzia tarehe 23 - 25 Oktoba 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia.
“Ziara hii ni ya kwanza ya Kitaifa ya Mheshimiwa Rais kufanya nchini Zambia tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022, itakumbukwa kuwa Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umejengwa na misingi ya kindugu,” alisema Waziri Makamba.
Mhe. Waziri Makamba amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia pia amepewa heshima ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tarehe 25 Oktoba, 2023 na anakuwa kiongozi mashuhuri wa wanne kuhutubia Bunge hilo.
“Mhe. Rais katika ziara hii amepewa heshima kubwa ya kuhutubua Bunge la Jamhuri ya Zambia, hii ni heshima kubwa na ya kipekee kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwani anakuwa mgeni mashuhuri wa nne kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tangu mwaka 2012,” Alisema Waziri Makamba
Waziri Makamba aliongeza kuwa ziara hiyo inalenga kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu na kuongeza kuwa katika ziara hiyo Mhesimiwa Rais Dkt. Samia na Mwenyeji wake watajadili namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la TAZAMA, Reli ya TAZARA na barabara ya TANZAM.
Aidha, malengo mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Dar es Salaam.
Akielezea kuhusu urari wa biashara kati ya Tanzania na Zambia, Mhe. Waziri Makamba amesema mwenendo wa ukuaji wa Biashara kati ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022.
0 Comments