Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NGO’s) kuwajibika kutunza na kulinda maadili kwa kuheshimu mila, desturi na tamaduni za kitanzania wakati wa utekelezaji wa programu mbalimbali.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifunga Jukwaa la Tatu la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) llililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Aidha amewataka kuzingatia sheria za nchi na kufuata miongozo mbalimbali inayoratibu shughuli za mashirika hayo.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa NGO’s kuhakikisha hazitumiki kuharibu maadili ya Tanzania kwa kutekeleza ajenda binafsi zisizofaa.
Ametoa wito kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii kufanya uchambuzi makini wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuishauri serikali ipasavyo juu mwenendo na ufanisi wa mashirika hayo.
Pia Makamu wa Rais amesema suala la mabadiliko ya tabianchi linapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika.
Amesema serikali Serikali ingependa kuona ushiriki zaidi wa NGOs katika utoaji elimu na hamasa kuhusu uhifadhi wa mazingira, udhibiti wa majanga na maisha endelevu, utunzaji wa misitu na uoto wa asili na kuchangia katika utengenezaji au uboreshaji wa sera mbalimbali.
Aidha amesema mashirika hayo yana nafasi ya kubuni programu muhimu kama ukusanyaji na urejelezaji taka, biashara ya kaboni, uanzishwaji na utunzaji wa vitalu vya miti na usambazaji wa miche pamoja na usafi wa mazingira katika maeneo maalum.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu zaidi.
Ametaja miongoni mwa hatua ambazo Serikali imechukua katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ni pamoja na kuandaliwa kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara (2020), Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020), Kitabu cha Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa (2020/2021/2022), pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2022/23 – 2026/27).
Hatua nyingine ni uanzishwaji wa madawati ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika Wizara za Kisekta na Mfumo wa Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambao imezinduliwa.
Kwa Upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima amesema NGO’s zimekuwa zikiunga mkono jitihada za serikali kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali ikiwemo miradi ya afya, elimu, mazingira, kilimo , maji, utawala bora, nishati na uwezaji wa jamii.
Ameongeza kwamba utekelezaji wa miradi hiyo umechangia kuboresha utoaji huduma, kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya serikali na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Dkt. Gwajima amesema Wizara itaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa NGO’s ili ziweze kuisadia jamii kwa kuzingatia mipango, mikakati na vipaumbele vya taifa.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Dkt. Liliani Badi ameiomba serikali kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo upatikanaji wa vibali kwaajili ya utekelezaji wamiradi na afua mbalimbali katika mikoa na halmashauri mbalimbali, vigezo vya upatikanaji wa misamaha ya kodi pamoja changamoto ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa kutozingatia utekelezaji wa takwa la kisheria la kuyajengea uwezo mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani ya nchi.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
05 Oktoba 2023
Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Vickness Mayao wakati alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma kushiriki Kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. (Tarehe 05 Oktoba 2023)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. (Tarehe 05 Oktoba 2023).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha tuzo aliyokabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) wakati wa Kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. (Tarehe 05 Oktoba 2023).
0 Comments