******************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WANANCHI wanaomiliki silaha kinyume na sheria mkoani Tanga wametakiwa kutii sheria bila shuruti na kuzisalimisha kwa jeshi la polisi kwani zoezi hilo litafikia mwisho ifikapo November 31 mwaka huu ambapo badala ya siku hiyo sheria kali itachukuliwa dhidi ya atakayekutwa anamiliki.
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi ametoa wito huo wakati matembezi maalumu ya kulinda amani ya jeshi hilo na kusema kuwa muda ambao umetolewa ili kila aliyenayo aisalimishe ili hatua isichukuliwe dhidi yake.
"Niwatake wananchi katika Mkoa wa Tanga, Wilaya zote, hata kama ndugu yako alikuwa anamiliki na amefariki inapaswa kuletwa polisi na kusalimishwa, lakini pia mtu kama anayo silaha na anajua kuwa anaimiliki isivyo halali aisalimishe kituo cha polisi au katika ofisi za watendaji hawatashtakiwa,
"Katika kipindi hiki ambacho Waziri wetu wa Mambo ya ndani ya nchi ametoa msamaha wa kuwasamehe wanaosalimisha silaha kwa hiari, lakini kwa watakaokaidi, niwatangazie kabisa kuwa kutakuwa na msako mkali usiokoma kwa maana wapo watu wanatengeneza silaha kama magobole halafu wanayatumia kufanyia uhalifu" amesema.
Kamanda Muchunguzi amebainisha kwamba kumekuwa na kesi za mara kwa mara kuhusu wanaojihusisha na utengenezaji wa magobole katika maeneo ya vijijini jambo ambalo limekuwa likiendelea bila watu hao kuwa na woga huku wakiendelea kusababisha matukio ya kihalifu.
Aidha amefafanua kwamba kwa sasa bado jeshi hilo linaendelea kufanya msako kuhusu uingizwaji wa madawa ya kulevya na tayari baadhi ya watumiaji wameshatiwa mbaroni lakini wanaohitajika zaidi ni wale ambao wanauza kwani bila kuwakamata wao biashara hiyo haitakoma.
"Mpango wa kudhibiti dawa za kulevya tunaendelea nao na tayari wapo watu wameshakamatwa, Mkoa wetu ni njia ya kupitishia lakini tunapokamata watumiaji tu haitoshi, inatupasa tupambane na wale wakubwa ambao ni wauzaji ili tuweze kukomesha vitendo hivi" amebainisha.
"Baadhi yao tuna majina yao, sasa niwaambie tu wajisalimishe hata kwa kujitetea, lakini kwa watakaendelea msako wetu utakapompitia kitakachotokea ni maumivu kwake kwakuwa amekataa kutii sheria bila shuruti" amesema.
Hata hivyo Kamanda ametoa wito kwa wananchi juu ya kulinda amani bila kusita kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi hilo katika kuwafichua wahalifu ili kuweza kuweka Mkoa katika hali ya ulinzi na usalama.
"Wale wote wanaoona wataweza kufanya uhalifu katika Mkoa wa Tanga, niseme hawataweza maana tutawashuhulikia ipasavyo kwa mujibu wa sheria, kikubwa tu niwaombe wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili tuweze kukomesha uhalifu" amesisitiza.
0 Comments