Kampuni ya SUMA JKT imetakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo Ofisi ya Makamu wa Rais unaoendelea katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya jengo hilo Oktoba 23, 2023.
Dkt. Yonazi ameiomba Ofisi ya Makamu wa Rais kusimamia kwa ukaribu ujenzi huo ili jengo hilo liweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora kuwawezesha watumishi kulitumia.
“Tuna imani na SUMA JKT lazima tuonedshe hata kampuni za ndani hasa hiz za umma zina uwezo wa kujenga na hatutegemei kuona mnafanya kazi ambayo hairidhishi, tunataka kuona kazi nzuri..tiles zimenyooka, rangi imekaa mahali pake,“ amesisitiza.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amehimiza usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi wanaojenga majengo hayo ikiwemo kupewa vifaa na elimu ya kujilinda dhidi ya majanga yanayoweza kutokea wakati wanaendelea na kazi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo uko nyuma kwa takriban siku 83.
Mitawi amefafanua kuwa kutokana na uchelewaji huo, mshitiri ambaye ni Ofisi ya Makamu wa Rais iliwaelekeza wawasilishe mpango kazi wa namna gani wanaweza kuzifidia siku hizo zilizopotea.
Hata hivyo amesema wataendelea kuwasimamia kwa ukaribu kuhakikisha kazi ya ujenzi wa jengo hilo lenye thamani ya shilingi bilioni 18.8 inakamilika kwa ubora unaotakiwa.
Mkataba wa ujenzi wa jengo hilo chini ya Msimamizi Elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ulisainiwa Oktoba 13, 2021 jijini Dodoma huku ukitarajiwa kukamilika Novemba 2023.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge
na Uratibu), Dk. Jim James Yonazi akisisitiza jambo wakati alipokagua maendeleo
ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais linalojengwa katika Mji wa
Serikali Mtumba jijini Dodoma Oktoba 23, 2023.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge
na Uratibu), Dk. Jim Yonazi akiendelea na ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi
wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini
Dodoma Oktoba 23, 2023.
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu
wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi (mwenye tai) na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi wakifuatilia taarifa ya ujenzi
kutoka kwa Mhandisi Julian Nicolaus walipotembelea ujenzi jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais
linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Oktoba 23, 2023.
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa
Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi (mwenye tai) akimsindikiza Katibu Mkuu, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi baada ya kumaliza ziara
yake ya kutembelea jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais linalojengwa katika Mji wa
Serikali Mtumba jijini Dodoma Oktoba 23, 2023.
Mwonekano kwa nje jengo la Ofisi ya Makamu wa
Rais linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambapo Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi amefanya
ziara ya kulikagua Oktoba 23, 2023.
0 Comments