Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT.MPANGO -SERIKALI ITAENDELEA KUFANYA KAZI NA KUSHIRIKIANA NA KANISA KATOLIKI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali itaendelea na kufanya kazi na kushirikiana vema na Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu mengine ya dini hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa mapokezi ya Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican alipopewa hadhi ya Ukardinali.

Amempongeza Kardinali Rugambwa kwa kuendelea kuhubiri amani na umoja wa Watanzania na kumsihi kuendelea kuwa chachu ya amani, upendo na umoja. Makamu wa Rais amesema ni baraka kwa Taifa la Tanzania kupata Kardinali wa tatu.

Kwa upande wake Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa amewaomba watanzania wa kila dini kuendelea kumuombea ili aweze kufanya vema kazi hiyo kwa uaminifu na kuweza kuleta maendeleo ya mwanadamu kwa ujumla kuanzia hapa nchini kimwili na kiroho na baadaye hata nje ya nchi.

Kardinali Rugambwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kanisa, Serikali na watanzania wote waliomtia moyo na kumtumia jumbe mbalimbali za pongezi zilizompa moyo na kumuimarisha.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

06 Oktoba 2023

Dar es salaam.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa pamoja na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki wakati wa Mapokezi ya Kardinali Rugambwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Vatican alipopewa hadhi ya Ukardinali. (Tarehe 06 Oktoba 2023)

Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa akizungumza na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki mara baada ya kuwasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Vatican. (Tarehe 06 Oktoba 2023).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa,Maaskofu pamoja na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki wakati wa mapokezi ya Kardinali Rugambwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. (Tarehe 06 Oktoba 2023).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifurahia jambo na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa mara baada ya kumpokea alivyowasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican. (Tarehe 06 Oktoba 2023).

Post a Comment

0 Comments