Ticker

6/recent/ticker-posts

BENKI YA NBC YASISITIZA DHAMIRA YAKE KUSAIDIA UKUAJI TEHAMA MASHULENI, YATOA MSAADA WA KOMPYUTA SEKONDARI MAKOKA

Dar es Salaam: Oktoba 13, 2023: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuwekeza zaidi kwenye ustawi wa sekta ya TEHAMA hususani kwa kuanzia katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake za kuboresha hali ya elimu nchini sambamba na kuandaa jamii itakayoweza kutumia kwa ukamilifu huduma mbalimbali za kidigitali zinazotolewa na benki hiyo.

Dhamira hiyo imesisitizwa na Meneja Maendeleo Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Mlimani City jijini Dar es Salaam Bw Eliezer Kabango wakati akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya Shule ya Sekondari ya Makoka iliyopo Kata ya Makuburi, wilayani Ubungo, Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye viunga vya shule hiyo jana. Katika mahafali hayo benki ya NBC tawi la Mlimani City ilikabidhi kompyuta tano kwa uongozi wa shule hiyo.

“Katika orodha ya mahitaji mengi tuliyopokea kutoka uongozi wa shule hii tumeona kwanza tuanze na changamoto ya vifaa vya TEHAMA kwa kutoa msaada wa kompyuta hizi tano zitakazosaidia uongozi wa shule na walimu kuweza kuweza kutimiza wajibu kwa ufanisi zaidi hususani katika kuandaa mitihani, kazi zao za kiofisi na kiutawala lakini pia kompyuta hizi zitawasaidia hadi wanafunzi kupata nukuu za masomo na mafunzo ya tehama,’’ alibainisha.

Kwa mujibu wa Bw Kabango benki hiyo imeweka msisitizo kwenye sekta ya TEHAMA kutokana na uwekezaji mkubwa inayoendelea kuufanya kwenye huduma za kidigitali ikiwemo huduma ya NBC Connect ambayo huwezesha huduma salama za kibenki kufanyika sehemu yoyote, muda wowote kwa njia ya mtandao.

“Tunaamini kwamba hawa wanafunzi ndio wateja wetu wakubwa wa kesho. Hivyo basi ili ili waweze kutumia huduma zetu kwa ukamilifu na kuzifurahi lazima wawe wameandaliwa kwenye eneo hili la matumizi ya TEHAMA. Kufanikisha hili sisi kama benki tunaendelea kutumia vema nafasi hizi kusaidia vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa taasis za elimu na vyuo mbalimbali,’’ aliongeza.

Zaidi Bw Kabango aliwasihi wazazi walioshiriki mahafali hayo kujenga utamaduni wa kuwakatia watoto wao Bima ya elimu itakayo wahakikishia uhakika wa kupata elimu bora hata pale wazazi wanaposhindwa kutimiza wajibu huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ulemavu wa kudumu au kifo.

“Bima ya Elimu itawawezesha wazazi kuwa na uhakika na elimu ya watoto wao kwa kuwa mtoto ataweza kusoma kwa kipindi chote cha masomo yake hadi atakapomaliza hata kama wazazi watapatwa na majanga yanayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo.’’ Alisema.

Akitolea mfano wa bima ya elimu ya Educare inayotolewa na benki hiyo, Bw Kabango alisema kupitia huduma hiyo mzazi humwekea akiba mtoto wake kidogo kidogo kwa ajili ya elimu kwa kiasi atakachopanga kwa mkataba wa muda kuanzia miaka saba hadi 18 ili kugharamia elimu ya mtoto wake.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Bw Emmanuel Wamahe pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo alisema kupitia msaada huo shule hiyo imefanikiwa kutatua changamoto ya TEHAMA kutokana na uhaba mkubwa wa kompyuta uliokuwa ikiikabili shule hiyo.

“Kwa kweli tumefarijika sana kwa msaaada huu uliotolewa na benki ya NBC. Naamini kupitia kompyuta hizi walimu wangu sasa wataweza kuandaa mitihani yao na majaribio kwa ubora zaidi. Pia wanafunzi watapata fursa ya kujifunza mambo ya msingi kupitia kompyuta hizi. Tuliwasiliasha maombi mengi zaidi ila tunashukuru sana kuona kwamba wameanza na hili tunatarajia mengi zaidi kutoka NBC’’ alisema

Akizungumzia hatua ya benki hiyo Mgeni Maalum kwenye mahafali hayo Bw Issa Ahmed ambae ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Makuburi alisema taasisi binafsi zinawajibu wa kushirikiana na serikali katika kuboresha upatokanaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu huku akiipongeza benki ya NBC kwa msaada huo.

“Zaidi pia niendelee kuwasisitiza wazazi kwamba wakati serikali na wadau kama NBC wanapambana kuboresha elimu ni vema nanyi mtambue umuhimu wa hili kwa kuwa elimu ni urithi pekee usio hamishika kwa mwanadamu. Na lengo kuu la elimu ni kuhakikisha kwamba mwanadamu anapata maendeleo endelevu maishani ili aweze kulinda na kudumisha utu wake na jamii inayomzunguka.’’ Alisema.
Meneja Maendeleo Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Mlimani City jijini Dar es Salaam Bw Eliezer Kabango (Kulia) akikabidhi moja ya kompyuta zilizotolewa na Benki hiyo tawi la Mlimani City kwa uongozi Shule ya Sekondari Makoka iliyopo kata ya Makuburi, Wilayani Ubungo Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake za benki hiyo kuboresha hali ya elimu nchini sambamba na kuandaa jamii itakayoweza kutumia kwa ukamilifu huduma mbalimbali za kidigitali zinazotolewa na benki hiyo. Anaepokea ni Mkuu wa Shule hiyo Bw Emmanuel Wamahe akishuhudiwa na Afisa Elimu wa Kata hiyo Bi Sabinadorothy Mapunda (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hiyo Bw Gasper Mujuni (wa pili kushoto). Makaadhiano hayo yalifanyika wakati wa Mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Makoka iliyopo kata ya Makuburi, Wilayani Ubungo Dar es Salaam sambamba na uongozi wa shule hiyo wakifurahia moja ya kompyuta zilizotolewa na benki ya NBC tawi la Mlimani City kwa shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake za benki hiyo kuboresha hali ya elimu nchini sambamba na kuandaa jamii itakayoweza kutumia kwa ukamilifu huduma mbalimbali za kidigitali zinazotolewa na benki hiyo.
Meneja Maendeleo Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Mlimani City jijini Dar es Salaam Bw Eliezer Kabango (aliesimama) akizungumza kwenye mahafali hayo.



Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wahitimu na wanaobaki pamoja na maonyesho ya kitaaluma.
Mmoja wa viongozi wa skauti Shule ya Sekondari Makoka (Kulia) akithibitisha ubora wa fimbo zinazotumiwa na vijana hao kwenye mapigano ya kupima ukakamavu ya mbele ya Meneja Maendeleo Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Mlimani City jijini Dar es Salaam Bw Eliezer Kabango huku wageni wengine pia wakishuhudia.
Meneja Maendeleo Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Mlimani City jijini Dar es Salaam Bw Eliezer Kabango (Katikati) akikabidhi cheti cha kuthibitisha uhitimu wa elimu ya Sekondari kwa mmoja wa wahitimu wa Shule ya Shule ya Sekondari Makoka iliyopo kata ya Makuburi, Wilayani Ubungo Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Meneja Maendeleo Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Mlimani City jijini Dar es Salaam Bw Eliezer Kabango (Katikati) akipokea kipande cha keki ya heri kutoka kwa mmoja wa walimu wa Shule ya Shule ya Sekondari Makoka iliyopo kata ya Makuburi, Wilayani Ubungo Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Shule hiyo Bw Emmanuel Wamahe (Kushoto) na Mgeni Maalum kwenye mahafali hayo Bw Issa Ahmed (kulia) ambae ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Makuburi.

Post a Comment

0 Comments