Ticker

6/recent/ticker-posts

Benki ya NBC Yazindua Msimu wa Tatu wa Kampeni ya "Wekeza NBC Shambani Ushinde’’, Kuchochea Kasi ya Kilimo cha Korosho Mtwara, Lindi

Mtwara: Oktoba 5, 2023: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua msimu wa tatu wa kampeni yake maalum kwa wakulima wa zao la korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi inayofahamika kama 'Wekeza NBC Shambani Ushinde’ ikilenga kuchochea kasi ya uzalishaji wa zao hilo kupitia huduma za kibenki mahususi zinazoendana na mahitaji ya wakulima hao. Zaidi, hatua hiyo inatajwa kuwa inalenga kuunga mkono na kufanikisha adhma ya serikali ya kuzalisha tani 700,000 za zao hilo kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameongoza hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika mkoani humo leo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa zao hilo wakiwemo viongozi wa kiserikali, viongozi vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika maofisa wa benki wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo wa Wakubwa wa benki hiyo, Bw Elibariki Masuke pamoja na wakulima wa zao hilo mkoani Mtwara.

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Kanali Abbas alisema imekuwa na mchango mkubwa kwa wakulima kutokana uwekezaji mkubwa wa elimu ya fedha uliombatana na kampeni hiyo sambamba na aina ya zawadi zinazolenga kuchochea kasi ya uzalishaji wa zao hilo ikiwemo zawadi kubwa za matreka.

“Kampeni hii ikiwa kwenye msimu wake wa tatu, binafsi nimeona mabadiliko yenye tija miongoni mwa wakulima ambayo naamini kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya kampeni hii ambayo kimsingi mkakati wake haulengi faida za kimasoko pekee bali pia inaunga mkono jitihada za serikali kukuza sekta hii muhimu na zaidi inalenga kumkomboa mkulima. Wito wangu kwa wakulima wa korosho mkoa wa Mtwara na Lindi tuendelee kuwaunga mkono NBC kwenye hili,’’ alisisitiza.

“Hata hivyo pia msisitizo wangu kwa wakulima unaendelea kuwa kwenye suala zima la nidhamu ya fedha wanazopata na kutumia vema mafunzo yanayotolewa na benki ya NBC kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba, matumizi ya bima mbalimbali ikiwemo bima ya afya pamoja na kuwekeza kwenye zana za kisasa za kilimo.’’ Aliongeza Kanali Abbas.

Kwa upande wake Bw Masuke alisema msimu wa tatu wa kampeni hiyo ya miezi mitatu ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kuitikia wito wa Serikali wa kuchangia katika kufanikisha agenda 10/30 ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia tano hadi kumi ifikapo mwaka 2030 ambapo kupitia kampeni hiyo benki inatoa zawadi kwa wakulima ili kuongeza motisha na ufanisi wao katika uzalishaji mashambani.

“Lakini pia, kampeni hii inakwenda sambamba na mafunzo ya huduma za kifenda, kama vile bima, uwakala, huduma za kidigitali, mikopo ya zana za kilimo, ujenzi wa maghala, na kusaidia shughuli za Amcos katika maandalizi ya msimu na masoko ya mazao, ikiwa ni pamoja na zao la Korosho.’’

“Tunashukuru kuona kwamba kampeni zetu mbili za awali zimekuwa na matokeo mazuri sana ambapo tulifanikisha ufunguaji wa akaunti za wakulima wa korosho zaidi elfu 50, AMCOS 140, na kutoa zana za kilimo kwa wakulima wa Korosho zaidi ya 250, ikiwamo pikipiki, Guta (Toyo) Spray Pump, baisikeli, na trekta kama sehemu ya zawadi kwa wakulima wetu wa zao hili la korosho.’’ Alitaja.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa alisema inawalenga wakulima wote wakiwemo mmoja mmoja, vyama vya ushirika na vyama vya msingi vya mazao ambao watapitisha fedha za mauzo kwenye akaunti za NBC Shambani.

“Kila mkulima aliye na akaunti na anayendelea kuweka pesa atapata nafasi ya kuingia kwenye droo ya ushindi ya kampeni hii. Mkulima atakayeweka fedha nyingi ataingia kwenye droo ya kujishindia zawadi kama Simu janja ‘Smartphone’, Pampu za Kupulizia dawa na TV.’’

‘’Kwa AMCOS na Union watakaokuwa na fedha nyingi, watapata nafasi ya kuingia kwenye droo ya kujishindia Pia Pikipiki, kompyuta mpakato ‘laptop’, Mizani za kidijitali na Trekta hususani kwa maeneo ya Lindi, Mtama na Kilwa’’ aliongeza.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara Bw Kakozi Ibrahimu walionyesha kuguswa zaidi na aina ya zawadi na elimu kuhusu fedha inayotolewa kupitia kampeni hiyo wakibainisha kuwa inawasaidia sana wakulima ambao hapo awali licha ya kupata fedha nyingi kupitia mauzo ya zao la korosho bado hazikuwasaidia kujikwamua na umaskini .

Wakizungumzia kampeni hiyo viongozi wa AMCOS katika mikoa hiyo walisema imekuwa na tija kubwa kwa wakulima huku wakionesha kuvutiwa zaidi na suala la kutokuwepo kwa makato ya fedha zao pindi wanapopitisha fedha hizo kupitia akaunti zao za NBC Shambani.

“Pamoja na uwepo wa zawadi mbalimbali kwenye kampeni hii ambazo kimsingi zitavutia wakulima wengi zaidi kujiunga na benki ya NBC zaidi tunavutiwa na kutokuwepo kwa makato ambayo yamekuwa yakituumiza sana hasa sisi viongozi wa AMCOS pindi tunapopitisha fedha za wanachama wetu kupitia akaunti zetu…kupitia akaunti za NBC Shambani tunashukuru kuona kwamba changamoto hii imekwisha kabisa,’’ alisema Bw Siraji Mtenguka, Mwenyekiti Bodi Chama Kikuu Cha Ushirika wa wakulima Mtwara-Masasi (MAMCU).


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed (Katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa msimu wa tatu wa kampeni ya 'Wekeza NBC Shambani Ushinde’ ya benki ya NBC maalum kwa wakulima wa zao la korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi ikilenga kuchochea kasi ya uzalishaji wa zao hilo kupitia huduma za kibenki mahususi zinazoendana na mahitaji ya wakulima hao. Hafla ya uzinduzi huo imefanyika mkoani Mtwara leo. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Kanali Patrick Sawala (wa tatu kulia), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile (Kulia), Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo wa Wakubwa wa benki hiyo, Bw Elibariki Masuke (wa tatu kushoto), Mwenyekiti Bodi Chama Kikuu Cha Ushirika wa wakulima Mtwara-Masasi (MAMCU) Bw Siraji Mtenguka wa pili kulia) na viongozi wengine waandamizi wa mkoa na benki hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo wa Wakubwa wa benki hiyo, Bw Elibariki Masuke (pichani) alisema msimu wa tatu wa kampeni hiyo ya miezi mitatu ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kuitikia wito wa Serikali wa kuchangia katika kufanikisha agenda 10/30 ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia tano hadi kumi ifikapo mwaka 2030 ambapo kupitia kampeni hiyo benki inatoa zawadi kwa wakulima ili kuongeza motisha na ufanisi wao katika uzalishaji mashambani.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed (Katikati) sambamba na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Shadida Ndile (Kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo wa Wakubwa wa benki hiyo, Bw Elibariki Masuke (kushoto) wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed (wa tatu kushoto) akisalimiana na Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed (wa pili kushoto) akisalimiana na Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Mtwara Bi Editha Mwakatobe wakati wa hafla hiyo.
Meneja wa Benki ya NBC tawi la Masasi Bw Eric Mbeyale akiwasilisha mada kuhusu kampeni hiyo kwa wakulima.
Baadhi ya wakulima wa korosho kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mtwara wakifuatilia uzinduzi guo
Baadhi ya zawadi zitakazotolewa kwa washindi mbalimbali wa kampeni hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa zao korosho mkoani Mtwara wakiwemo viongozi wa kiserikali, viongozi vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika maofisa wa benki wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo wa Wakubwa wa benki hiyo, Bw Elibariki Masuke pamoja na wakulima.

Post a Comment

0 Comments