Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AACHA MAAGIZO MKOA WA TANGA, AFAFANUA JAMBO VITAMBULISHO VYA NIDA.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa uongozi wa Mkoa wa Tanga ili kuboresha miundombinu ya chuo cha uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo wilayani Mkinga huku akisisitiza mambo kadhaa kwa wahitimu wa mafunzo ya awali ya jeshi hilo.

Waziri Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akifunga mafunzo ya awali kozi namba 1, 2023 katika viwanja vya chuo hicho ambacho kilifunguliwa rasmi mwaka 2020 lakini bado miundombinu yake bado haijakamilika kwa kiasi fulani na kwamba umaliziaji wa ujenzi huo utaendelea kufanyika kidogo kidogo kulingana na upatikanaji wa fedha.


Majaliwa amezitaka Mamlaka za maji, Tanga Uwasa pamoja na Ruwasa wilayani humo na Mkoa kwa ujumla kuhakikisha wanafikisha huduma ya maji yenye uhakika wa kupatikana wakati wowote lakini pia aliiagiza TARURA kuangalia jinsi ya kufanya matengenezo na kuweka lami kwenye barabara inayokwenda chuoni hao kitokea barabara kuu ya Horohoro.


"Nimesikia kero zenu hapa chuoni, kwanza barabara inayoingia chuoni kutoka barabara kuu, lakini pia za humu ndani pamoja na uwanja wetu wa gwaride havina lami, nianze kumuelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga pamoja na Wilaya ya Mkinga kutengeneza barabara inayoingia kwenye chuo chetu kwa kiwango cha lami",


"Kipande cha km 2 hakitamishinda kuweka lami, nataka mwakani nikija hapa nipite juu ya lami, na kuhusu barabara za ndani pamoja na uwanja, hili ni la Wizara ndiyo wanahusika, wekeni kwenye bajeti ili mkamilishe eneo hili" amesema Majaliwa.


"Kuhusu kero ya maji ndani ya chuo na vijiji jirani, Mamlaka za maji Mkoa wa Tanga pamoja na RUWASA Mkinga hakikisheni kuwa Taasisi hii inaunganishwa kwenye mtandao wa maji, lakini pia nimuagize Katibu Mkuu uko hapa, unao uwezo wa kuwaunganishia wana chuo tanki kubwa linalotosha kwa idadi ya wanaokusudiwa kuja kukaa hapa pamoja na wakufunzi wao ili wapate maji safi na salama na ya uhakika wakiwa hapa" amesisitiza.


Eneo lingine lenye kero ni kuhusu ukosefu wa jengo la mama na mtoto hapa chuoni ambapo Waziri mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaiingiza zahanati hiyo katika migao ya vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma hiyo ili wanakijiji wanaokwenda kupata tiba waweze kupewa huduma stahiki.


"Kwakuwa chuo hiki kina zahanati na inatoa huduma ya msingi ya afya ya mama na mtoto, hivyo basi Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Mkinga pamoja na Mganga mkuu wa Wilaya, kwenye migao yenu ya vituo vya afya ambavyo vimekuwa na eneo la jengo la mama na mtoto, eneo hili pia ni muhimu ili pamoja na vijiji vya jirani viweze kupata huduma bora hapa chuoni" amesema.


"Haya maelekezo ninayoyatoa tusije tena mwakani tukaja kuzungumza tena mambo haya, nataka nikija hapa nikute jengo la mama na mtoto, lakini pia kuwepo na vipimo na tiba, na hata vyumba vya wakinamama kujifungulia ili hawa makamanda wetu waweze kupata huduma hizo hapa hapa chuoni" amesisitiza.


Aidha amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha anaongea na Waziri wa Fedha ili kuweza kukamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba za Maofisa wa Uhamiaji zikiwemo za wakufunzi ambazo zinahitajika zijengwe kwenye eneo hilo, hivyo uharakishwaji wa upatikanaji wa fedha unahitajika.


"Waziri wa Mambo ya Ndani, fanya mawasiliano na Waziri wa Fedha ili muhakikishe mnafanya mchakato wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi huu, na kwakuwa fedha hizi zilishakuwa zimepanngwa kwenye bajeti, sasa ni wakati wa kuelekeza kwenye chuo chetu ujenzi uanze na ukamilike, ili na wao wafanye kazi yao kwa utulivu" amebainisha.


Hata hivyo Waziri ametoa msisitizo kwa wanafunzi waliohitimu mafunzo yao, kwenda kuyatumia vema waliyojifunza katika kudhibiti wahamiaji wanaoibgia nchini hasa kwenye maeneo ya vipenyo, vituo na mipakani.


"Sina mashaka na ninyi, mmeonesha ukakamavu wa hali ya juu, nina imani hamtachoka kufuatilia vipenyo na kuwabaini wale wote wanaoingia nchini bila kufuata utaratibu, lakini pia mwende mkafanye kazi kwa uzalendo na weledi huku mkitanguliza kwanza maslahi ya nchi letu, kazi yenu ni kulilinda Taifa hili".


Alibainisha kwamba kufuatia kuongezeka kwa tekinolojia za kisasa na makosa mbalimbali ya kiuhalifu hususani biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, "kila mmoja ahakikishe kwamba anapata maarifa mapya mara kwa mara ili aweze kukabiliana na mabadiliko hayo" amesisitiza.


"Kila kamanda akazingatie maadili na miiko ya kazi na akawe mfano bora wa uadilifu kwa jamii inayomzunguuka, vilevile kwa atakayebainika anafanya vitendo viovu ikiwemo rushwa, wizi wa maduhuli ya serikali au kujiunga na mitandao ya kiuhalifu na ukiukwaji wa nidhamu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake".

Kutokana na jukumu walilonalo Idara ya Uhamiaji, pia Waziri ametoa angalizo kwa wanaolinda mipaka ya nchi kuhusu suala la wahamiaji haramu huku akifafanua kuhusiana na vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipaka.

"Naomba niongeze kwamba, Wana Mkinga na wananchi wote waliopo maeneo ya mipakani, kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Taasisi yetu (NIDA) ni usalama wa Taifa letu, kwahiyo anayetakiwa kupewa ni lazima awe Mtanzania tu,

"Na nataka niwahakikishie wananchi wote, kama wewe ni Mtanzania kitambulisho kile lazima utakipata, tatizo linalojitokeza katika maeneo ya mipakani ni muingiliano tulionao ni Jumuia yetu ya Afrika Mashariki na nchi jirani ambao sisi tayari tumeshauenda na wao wameshauingia,


"Lakini wapo wanaoingia na wanatamani kupata kitambulisho kile ili akiwa Tanzania awe kama Mtanzania, hilo ni kosa na haiwezekani apate kitambulisho cha Taifa letu na wapo wengine pia ambao wanajua kuzungumza kiswahili na wanataka kujiita Watanzania" amebainisha Majaliwa.


Amesisitiza kwamba, ili kuondokana na tatizo la kusambaa kwa kitambulisho cha Taifa kama ambavyo kilisambaa cha mpiga kura ni lazima nchi kuwa makini na kufanya uhakiki wake ili kuwawezesha wananchi wote ambao wana uhalali wa kuwa na vitambulisho hivyo waweze kuvipata.


"Nataka niwahakikishie Watanzania, tumeongeza umakini, tunachokifanya hivi sasa, tumeongeza timu ya uhakiki kutoka jeshi letu la uhamiaji ili kutambua uraia wao, lakini pia tumeongeza idadi ya watumishi kwenye Wilaya zote na Taasisi zetu za NIDA ili kukamilisha huo uhakiki ili kuwawezesha Watanzania kupata vitambulisho hivi" amesema.

Post a Comment

0 Comments