Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewahimiza wakuu wa mikoa kusimamia ajenda ya usafi wa mazingira kila Jumamosi asubuhi ili kuifanya miji kuwa safi.
Pia, ameelekeza kila mwananchi ashiriki kikamilifu kufanya usafi katika eneo linalozunguka nyumba yake ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuongoza zoezi la usafi wa mazingira kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani katika soko la machinga jijini Dodoma leo Septemba 2023.
Amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa zinasimamia kikamilifu usafi wa mazingira katika masoko yaliyopo katika maeneo yao unakuwa wa kudumu.
Waziri Jafo amewaelekeza watendaji wa mamlaka hizo kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa taka na kutupwa kwenye madampo yaliyopo katika maeneo yao bila kuzagaa ovyo.
“Kama mnavofahamu hapa nchini tunazalishaji takriban tani saba za taka lakini tani chache tu ndio zinatupwa dampo. Tunaadhimisha siku hii ya usafi kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya Tanzania yanakuwa safi na ndio maana tumeelekeza majiji na manispaa wanakuwa na mikakati ya kutenga bajeti kuhakikisha taka zinasombwa kila mara ili zisirundikane,” amesisitiza
Aidha, Dkt. Jafo ameupongeza uongozi wa Jiji la Dodoma kwa kusimamia vyema usafi wa mazingira kwa kuwa navitendea kazi vikiwemo magari na kutaka mamlaka zingine ziige mfano huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amnesema kuwa maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu Bonde la Mzakwe jijini humo yamefanyiwa kazi.
Amesema kuwa miti iliyopandwa imeanza kukua pamoja na miumdombimu ya kuzuia moto na operesheni kuwachukulia hatua wavamizi zinaendelea ili kuhakikisha eneo hilo linarudi katika uoto wa asili.
“Mheshimiwa Waziri sasa hivi tumeanza kukamata wanaoingiza mifugo na wanaochoma mkaa kwenye Bonde la Mzakwe na yote haya ni maelekezo ya Serikali kuhakikisha chanzo hicho cha maji kinatunzwa,” amesema.
Nae Mkurugenzi wa Shirika linalojishughulusha na mazingira la GO Plant Tanzania Bw. Emmanuel Likuda amesema wao kama wadau wana kila sababu ya kuungana na viongozi katika kuadhimisha Siku ya Usafi.
Bw. Likuda Amesema kuwa taka zinazalishwa kila wakati na hivyo ni jukumu la kila mwananchi popote pale alipo kujitokeza na kushiriki katika kufanya usafi kila wakati.
Amesema kuwa uchafu ni dalili ya kutokuwa na afya ya akili hivyo kama wadau wa mazingira wana kila sababu ya kujivunia kufanya usafi kama kielelezo cha afya ya akili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wananchi mara baada ya kuongoza zoezi la usafi wa mazingira kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani katika soko la machinga jijini Dodoma leo Septemba 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiongoza zoezi la usafi wa mazingira ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani katika soko la machinga jijini Dodoma leo Septemba 2023.Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisukumu toroli la taka kuzipeleka katika gari maalumu la kukusanyia taka wakati wa zoezi la usafi wa mazingira kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani katika soko la machinga jijini Dodoma leo Septemba 2023.
0 Comments