Ticker

6/recent/ticker-posts

WARAJIS WASAIDIZI VYAMA VYA USHIRIKA WATAKIWA KUSIMAMIA VYAMA KUJIENDESHA KIBISHARA


Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) Dkt. Benson Ndiege,akizungumza wakati akifungua Kikao kazi kati yake na Warajis Wasaidizi,Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Upili chenye lengo la kujadili Mwelekeo wa ushirika nchini kilichofanyika leo Septemba 11,2023 jijini Dodoma.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) Dkt. Benson Ndiege,akisisitiza jambo wakati wa Kikao kazi kati yake na Warajis Wasaidizi,Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Upili chenye lengo la kujadili Mwelekeo wa ushirika nchini kilichofanyika leo Septemba 11,2023 jijini Dodoma.


NAIBU Mrajis wa Vyama vya Ushirika – Udhibiti Bw. Collins Nyakunga,akitoa taarifa ya Kikao kazi kati Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Warajis Wasaidizi,Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Upili chenye lengo la kujadili Mwelekeo wa ushirika nchini kilichofanyika leo Septemba 11,2023 jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) Dkt. Benson Ndiege (hayupo pichani) wakati akifungua Kikao kazi kati yake na Warajis Wasaidizi,Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Upili chenye lengo la kujadili Mwelekeo wa ushirika nchini kilichofanyika leo Septemba 11,2023 jijini Dodoma.



Na.Alex Sonna-DODOMA

MRAJIS wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) Dkt. Benson Ndiege amewataka Warajis Wasaidizi wa vyama vya ushirika kuangalia namna ya kuanza kutekeleza Mfumo wa Stakabadhi ghalani ili kuuwezesha mfumo wa vyama vya ushirika kuweza kujiendesha kibiashara kwa ushindani na kuaminika.

Hayo ameyasema wakati wa Kikao kazi kati yake na Warajis Wasaidizi,Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika vya Upili kilicholenga kujadili muelekeo wa ushirika nchini kilichofanyika leo Septemba 11,2023 jijini Dodoma.

Maagizo haya ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akishiriki Mkutano wa kilimo Dar es Salaam ambapo alivitaka vyama vya ushirika nchini kuhakikisha kuwa wanatekeleza Mfumo wa Stakabadhi ghalani kwa mazao mengine ya biashara kama wanavyofanya kwenye zao la korosho na ufuta.

Dkt. Ndiege amesema kuwa ni wakati sasa vyama vya shirika vianze kuimarisha biashara ya mauzo ya mazo ya ushirika kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Kuna baadhi ya vyama katika mkoa wa Songwe, Manyara na mikoa ya Kusini wamefanya vizuri kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, kupitia mfumo huu bei ya ufuta imepanda kutoka sh 1,300 mwaka jana hadi kufikia sh 4,000 mwaka huu, tukitumia mfumo huu ushirika utajiendesha kibiashara na kuwa wenye tija kwa wakulima” alisema.

Aidha, amesema kuwa katika kuhakikisha Ushirika unakuwa na mwelekeo chanya ni lazima jitihada zifanyike ili kuhakikisha kunakwa na uwekezaji katika mifumo ya kisasa kidigitali kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika vyama pamoja na mamlaka za usimamizi.

“Mpaka sasa tumesajili vyama 5,642 na wanachama 704,648 katika Mfumo wetu wa MUVU ni lazima tuhakikishe vyama vyote 7,000 na wanachama tulionao zaidi ya milioni 8 wanasajiliwa katika mfumo huu ili shughuli zetu zote zifanyike katika mfumo wa kidigitali, lakini pia tuhakikishe mfumo huu unakwenda sambamba na Mizani ya kidigitali ili tuweze kwenda kisasa” amesema Dkt.Ndiege

Hata hivyo amewataka Warajis Wasaidizi kuhakikisha wanahakikisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika inayotarajiwa kuanzishwa rasmi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

“Tunahitaji bil 15 ili kuweza kuanzisha benki hii, mpaka sasa tuna bil 6.7 tukiwa na upungufu wa bil 8.3, ofisi yangu ilitoa waraka kwa ajili ya wanachama kuchangia ama kununua hisa ili waweze kumiliki hisa kwa pamoja na namna tunavyoweza kuwahamasisha ili wawe miongoni mwa wamiliki lakini pia tuweze kukamilisha kiwango kilichobaki ili benki yetu iweze kuanzishwa” amesema

Dkt. Ndiege amesema kuwa ili kuhakikisha ukuaji na maendeleo ya Ushirika ni lazima kuhakikisha usimamizi na udhibiti wa vyama hivi pamoja na kuhamasisha ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum ili kuhakikisha wananchi wengi Zaidi wananufaika.

“Tunaweza kuhamasisha ushirika katika miradi ya BBT, eneo la mbogamboga, mifugo na uvuvi pamoja na kuwahamasisha uanzishwaji wa SACCOS ndani ya AMCOS, kutoa elimu kupitia majukwaa ya ushirika ya mikoa pamoja na kuongeza uelewa wa umma kuhusu shirika kupitia vyombo vya habari” amesema Dkt. Ndiege

Dkt. Ndiege amesema kuwa ili kuimarisha shughuli za vyama vya ushirika pamoja na usimamizi kila mdau analojukumu la kuhakikisha kuwa ushirika unajibu mahitaji ya jamii kwa uimara wake na uendelevu kwa kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.

“Tunapaswa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutatua changamoto za ushirika pamoja na kuimarisha uwekezaji wa mali za ushirika katika uzalishaji” amesema

Post a Comment

0 Comments