Ticker

6/recent/ticker-posts

WAFUGAJI WAASWA KUCHANJA MIFUGO, KUEPUKA MAGONJWA

Wafugaji nchini wameaswa kuchanja mifugo yao ili kuikinga na magonjwa yanayoweza kuwasababishia hasara na kushusha uchumi wa familia na nchi kwa ujumla.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Mhe. Erasto Mpete Septemba 6, 2023 kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa Wafugaji, Wauzaji wa pembejeo za Mifugo pamoja na Maafisa Mifugo wa Halmasahuri za Miji ya Njombe na Makambako kwa lengo la kutoa elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo, utambuzi wa chanjo zinazozalishwa na Serikali pamoja na huduma zinazotolewa na TVLA.

“Kuchanja ni njia bora ya kuepuka magonjwa, na kwa sasa tupo kwenye karne ya sayansi na teknolojia, miaka 10 iliyopita hatukuwa na chanjo zilizokuwa zinazalishwa hapa nchini, chanjo zote zilikuwa zinatoka nje ya nchi, Serikali imefikia hatua ya kuzalisha chanjo kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambazo zinapatikana ndani ya nchini. Chanjo hizo zimeshaanza kutumika nchini na tumeona ufanisi wake kwa hiyo ni jukumu letu kwa kushirikiana na Serikali kutangaza chanjo hizi ili kukuza uchumi wa Taifa.”alisema Mhe. Mpete.

Sambamba na hilo, Mhe. Mpete ameitaka sekta ya Mifugo kuwahamasisha wafugaji kuzitumia chanjo zinazozalishwa nchini ili kuwa na uhakika wa afya za mifugo kama sehemu ya ukuzaji wa uchumi wa nchi, vilevile amewataka washiriki wote wa kikao hicho wakatoe elimu kwa wenzao ambao hawajafanikiwa kuhudhuria, na ni matarajio yake kuwa baada ya kikao hicho wafugaji wote waliopo Njombe na sehemu nyingine watapata elimu hiyo.


Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini (Iringa) Dkt. Geofrey Mbata alisema kuwa Wakala imejiwekea utaratibu wa kuzunguka kwenye Halmashauri zote kukutana na wadau wake hasa wafugaji, wauzaji wa pembejeo za mifugo pamoja na maafisa mifugo kwa lengo la kukumbushana matumizi sahihi ya chanjo za mifugo, kuelezea kwa undani huduma zinazotolewa na TVLA, kupanga mikakati na makubaliano, kufahamiana na kuimarisha mahusiano ya kikazi kwani wakiwafikia hao kutakuwa na soko la uhakika la nyama na mifugo nje ya nchi.

Dkt. Mbata alisema kuwa Majukumu makubwa ya TVLA ni pamoja na Kufanya uchunguzi na Utambuzi wa Magonjwa ya Wanyama, uzalishaji na usambazaji wa Chanjo za Mifugo, Uhakiki wa Ubora wa vyakula vya Mifugo, kusajili na kudhibiti ubora wa viuatilifu vya Mifugo, Kufanya tafiti zinazolenga kupata njia za kudhibiti magonjwa ya Wanyama na wadudu wanaoyaeneza pamoja na Huduma za ushauri na Mafunzo.

Akitoa elimu katika vikao kazi hivyo vilivyofanyika Halmashauri ya Mji wa Makambako na Njombe, Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Dkt. Charles Mayenga Ngassa alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye mifugo mingi, tukizalisha chanjo wenyewe, tunaepuka uwezekano wa kuingiza vimelea vya magonjwa mapya ambayo hayapo hapa nchini, kwani chanjo zinazotengenezwa nchini, zinatengenezwa kwa kutumia vimelea vinavyopatikana kwenye mazingira yetu,

Dkt. Ngassa aliongeza kuwa tukitumia chanjo zetu tunaifanya nchi yetu kuwa salama na vilevive tunamuwezesha mfugaji kuweza kununua chanjo kwakuwa zina gharama nafuu.

“Ukiwapa chanjo wanyama ambao wanaugua utakuwa umemsaidia mnyama wako kufa, ila ukiwachanja wakiwa na afya, ni vigumu kwa mnyama kushambuliwa na ule ugonjwa, chanjo inatolewa kabla mnyama hajaugua ili aweze kujitengenezea kinga.”

*“Watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya chanjo na dawa, chanjo inatolewa kabla ya mnyama kuugua ili ajiandae siku mdudu au kimelea anaesababisha ugonjwa akija yeye anakuwa tayari ana kinga ya kupambana nae ili mwili usiathiliwe na ule ugonjwa. Dawa ni kemikali ambazo zimeandaliwa na kufanyiwa majaribio na kuonekana kwamba mnyama ambae ni mgonjwa dawa hiyo inafanikiwa kuwaondoa wadudu wanaosababisha ugonjwa huo, na dawa ikishindwa kuviondoa mnyama huyo hufa au kupata changamoto kubwa ya kiafya.”* Alisema Dkt. Ngassa

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako Bwana Samweli Komba alisema kwamba Serikali inategemea uchumi wa nchi ukue kupitia mifugo, na kama hatuta wekeza kwenye kuilinda na kuipa huduma zote, uchumi wetu hautakua, vilevile ameishukuru Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kutoa elimu ya uchanjaji na utambuaji wa chanjo za Mifugo zinazozalishwa na Serikali hapa nchini, na amewataka watu wote waliopata elimu hiyo waache kufuga kwa mazoea na kuitumia elimu waliyoipata kwenda kuboresha afya za mifugo yao, na pale watakapopata changamoto, wawe wanawasilina na wataalamu wa TVLA waweze kusaidia kuzitatua.

Wakiongea katika nyakati tofauti, baadhi wa Maafisa Mifugo, Wamiliki wa Maduka ya Pembejeo za Mifugo pamoja na Wafugaji kutoka Halmashauri za Miji ya Njombe na Makambako wamesema kuwa wanaishukuru Serikali kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania kutoa elimu hiyo kwani kwa kipindi kirefu walikuwa wanashindwa kutofautisha chanjo halisi zinazozalishwa na Serikali pamoja na chanjo feki zinaotengenezwa na watu wasioitakia mema nchi yetu na wameahidi kuwa mabalozi na kutoa ushirikiano pale watakapopata viashiria vya chanjo feki.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmasahuri ya Mji wa Makambako Bwana Samweli Komba akifungua kikao kazi cha utoaji elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo, utambuzi wa chanjo zinazozalishwa na Serikali kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) pamoja na huduma zinazotolewa na (TVLA) kwa Maafisa Mifigo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo (hawapo pichani) wa Halmasahuri ya Mji wa Makambako kilichoandaliwa na TVLA Septemba 5, 2023.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini (Iringa) Dkt. Geofrey Mbata (aliesimama kulia) akitoa elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo pamoja na shughuli zinazofanywa na TVLA kwa Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo (hawapo pichani) wa Halmasahuri ya Mji wa Makambako kilichoandaliwa na TVLA Septemba 5, 2023.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Dkt. Charles Ngassa (aliesimama) akitoa elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo na namna ya kuzitambua chanjo zinazozalishwa na TVLA kwa Maafisa Mifigo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo (hawapo pichani) wa Halmasahuri ya Mji wa Makambako kilichoandaliwa na TVLA Septemba 5, 2023.
Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo ambao ni washiriki wa Kikao kazi cha utoaji elimu kilichoandaliwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo, utambuzi wa chanjo zinazozalishwa na Serikali pamoja na huduma zinazotolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kutoka Halmasahuri ya Mji wa Makambako wakipewa elimu kutoka kwa Meneja TVLA Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini (Iringa) Dkt. Geofrey Mbata (aliesimama kulia) na Meneja wa TVLA kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Dkt. Charles Ngassa (aliesimama kushoto) Septemba 5, 2023.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Mhe. Erasto Mpete akifungua kikao kazi cha utoaji elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo, utambuzi wa chanjo zinazozalishwa na Serikali pamoja na huduma zinazotolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo (hawapo pichani) wa Halmasahuri ya Mji wa Njombe kilichoandaliwa na TVLA Septemba 6, 2023.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Mhe. Erasto Mpete (kulia) akichangia mada kwenye kikao kazi cha utoaji elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo, utambuzi wa chanjo zinazozalishwa na Serikali pamoja na huduma zinazotolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo wa Halmasahuri ya Mji wa Njombe kilichoandaliwa na TVLA Septemba 6, 2023. Waliosimama kutoka kushoto ni Meneja wa Wa TVLA kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Dkt. Charles Ngassa na Meneja TVLA Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini (Iringa) Dkt. Geofrey Mbata
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini (Iringa) Dkt. Geofrey Mbata (aliesimama) akitoa elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo pamoja na shughuli zinazofanywa na TVLA kwa Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo (hawapo pichani) wa Halmasahuri ya Mji wa Njombe kilichoandaliwa na TVLA Septemba 6, 2023.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Dkt. Charles Ngassa (aliesimama) akitoa elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo na namna ya kuzitambua chanjo zinazozaliswa na TVLA kwa Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo wa Halmasahuri ya Mji wa Njombe kilichoandaliwa na TVLA Septemba 6, 2023.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Mhe. Erasto Mpete (kulia) akigawa chanjo ya Mdondo wa Kuku (Kideli) kwa Bi. Ichikael Malisa mmoja wa wafugaji wa kuku kwenye kikao kazi cha utoaji elimu kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo, utambuzi wa chanjo zinazozalishwa na Serikali pamoja na huduma zinazotolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa Maafisa Mifugo, Wafugaji na Wauzaji wa pembejeo za Mifugo wa Halmasahuri ya Mji wa Njombe kilichoandaliwa na TVLA Septemba 6, 2023.















Post a Comment

0 Comments