Ticker

6/recent/ticker-posts

UDSM YAZINDUA KONGAMANO LA KWANZA LA KIMATAIFA LA INSIA LA AFRIKA 2023

CHUO Kikuu Cha Dar es Salaam kupitia Ndaki ya Insia imezindua Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Insia la Afrika 2023 ambalo linajumuisha takribani nchi 17 kutoka sehemu tofauti wenye lengo la kutafakari mada mbalimbali za Insia katika kuangalia masuala ya kibinadamu na maendeleo kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi leo septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma Prof. Bonaventure Rutinwa amesema dhima kuu ya mkutano huo ni kuhakikisha mambo yote ambayo yanafanyika yawe ya kiuchumi, kisiasa yanabeba ubinadamu ndani yake ili kuipeleka tasnia hiyo ya insia katika ngazi nyingine.

"Mkutano huu umeandaliwa ikiwa ni sehemu ya kusherekea miaka 10 tangu kuanzia kwa ndaki ya insia, hivyo umuhimu wa mkutano ni kuwawezesha washiriki kutafakari mada mbalimbali zinazohusu insia ambayo ni mambo ya ubinadamu zaidi ili kuangalia katika mawanda mapana kuanzia kiuchumi, kisiasa, jinsia na maendeleo kwa ujumla " amesema Prof.Rutinwa.

Amesema matumaini yao kwa ushiriki wa watu kutoka sehemu mbalimbali kwenye kongamano hilo utawezesha kubadilishana maarifa, uzoefu ili kuipeleka tasnia hiyo ya insia katika ngazi nyingine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Prof. Gastor mapunda amesema ndaki ya insia imeendelea kufanya vizuri na kuwa miongoni mwa ndaki kubwa zaidi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanafunzi wengi wanafurahia kusoma kwenye ndaki hiyo.

Nae Rasi wa Ndaki ya Insia Dkt. Rose upor amesema washiriki zaidi ya 200 kushiriki wakiwemo 139 kutoka nchi 17 ndani ya Afrika na nje ya Afrika ili kujadili mustakabali mzima wa taaluma za kinsia zinapoelekea ambazo ni taaluma za falsafa na dini, turathi, isimu, malikale, fasihi ya lugha pamoja na historia.



Post a Comment

0 Comments