Ticker

6/recent/ticker-posts

TMDA YATOA MAFUNZO KWA HALMASHAURI KUONGEZA UFANISI UCHUNGUZI WA DAWA, MADHARA MATUMIZI YA CHANJO.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewajengea uwezo wataalamu wa Afya katika Halmashauri tano za Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya uchunguzi dawa pamoja na madhara yanayotokana na matumizi ya chanjo.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo timu za uchunguzi kutoka Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Mjumbe wa Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mikaji Rashid, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kusaidia timu za uchunguzi kufanya kazi kwa ufanisi.

Dkt. Rashid amesema kuwa elimu hiyo inakwenda kupeleka maarifa katika vituo vyao vya kazi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha wanafikia malengo.

"Timu zote za Halmashauri zinapaswa kuweka malengo ya ufatiliaji wa watumiaji wa dawa na matumizi ya chanjo pamoja na kutoa taarifa kwa Mamlaka husika" amesema Dkt. Rashid.

Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Dkt. Yona Hebron, amesema kuwa wameandaa mafunzo maalumu kwa ajili ya timu za uchunguzi wa dawa pamoja na madhara yanayotokana na matumizi ya chanjo.

Dkt. Hebron amesema kuwa timu zimeundwa kutoka kila halmashauri ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa pamoja madhara yanayotokana na matumizi ya chanjo.

Amesema kuwa kila timu itakuwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi.

Dkt. Hebron amesema kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuhakikisha wajumbe wa timu za uchunguzi wanajengewa uwezo wa kufanya uchunguzi wa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa na chanjo.

"Sheria inatutaka pale madhara yanapotokea uchunguzi unapaswa kufanyika ndani ya siku saba ili kuwezesha Mamlaka na Serikali kwa ujumla kuchukua hatua juu ya dawa ambayo imekuwa analeta shida katika matumizi yake" amesema Dkt. Hebron.

Amesema kuwa ni muhimu timu hizo kujengewa uwezo wa kufanya uchaguzi badala ya kusubiri watumishi wa TMDA kufanya uchunguzi katika maeneo yao ya kazi.

Amefafanua kuwa washiriki wa mafunzo haya wamepewa nyezo mbalimbali za kufanyia kazi pamoja na kujifunza namna ya kufatilia madhara yanayotokana na chanjo jambo ambalo ni rafiki katika kufanikisha utendaji kazi.

"Mafunzo yanakwenda kutusaidia katika kuhamasisha kutoa taarifa ya madhara yanayotokana na dawa pamoja na matumizi ya chanjo, hivyo kila halmashauri ikitimiza uwajibu wake tutafikia malengo tarajiwa" amesema Dkt. Hebron.

Post a Comment

0 Comments