Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) ni shirika la utafiti na maendeleo lililoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 5 ya 1979 na ilianza kufanya kazi tarehe 1 Aprili, 1979.
TIRDO imejikita katika kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kusaidia sekta ya viwanda nchini kwa kutoa utaalam wa kiufundi na huduma za usaidizi ili kuboresha zao msingi wa teknolojia.
Katika sekta ya Nishati, TIRDO wamejikita katika kufanya utafiti wa maendeleo na huduma za kiufundi kwenye viwanda michakato na matumizi sahihi na rafiki kwa Maendeleo ya Viwanda nchini.
Mpaka sasa TIRDO wamefanikiwa kuwa na Maabara bora na ya kisasa yenye uwezo wa kutoa huduma za ukaguzi wa mifumo ya nishati viwandani na kwenye majengo, kupima ubora wa majiko katika mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kutoa ushauri na mafunzo ya mpango bora wa menejimenti na utekelezaji wa matumizi bora ya nishati.
Mhandisi Augustino Masse kutoka TIRDO anasema kuwa mpango huu wa matumizi bora ya nishati ambao kwa hapa nchini unasimamiwa na Wizara ya Nishati umefanikiwa kwa kushirikiana na Jumuhia ya Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambapo malengo makuu ni kutoa elimu kwa watumiaji wakubwa wa umeme (Viwandani) hapa nchini pamoja na kutoa elimu juu ya aina za vifaa vinavyotumika majumbani na ofisini.
Mpaka sasa jumla wa watumiaji wakubwa wa umeme waliofikiwa na mradi huu ni pamoja na hospitali ya Agakhan, Kiwanda cha SILAFRICA na jengo la PSSSF yalipo Makao makuu ya UNDP barabara ya Sam Nujoma.
Mhandisi Masse anasema kuwa kati ya watumiaji hao watatu kiwanda cha SILAFRICA baada ya kupatiwa elimu na kufanyiwa ukaguzi wa ufanisi wa umeme wameweza kupunguza matumizi kutoka kVA 2889 mpaka 2008.71kVA ambapo wameweza kuokoa jumla ya fedha za kitanzania shilingi Milioni 44.05 kwa mwaka mmoja.
Kwa upande wake mtaalam wa umeme kutoka SILAFRICA Bw.Frank Mapunda anasema kuwa mpango huu wa matumizi bora umewasaidia kupunguza matumizi na kuepuka adhabu za kimatumizi kutoka kwa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na kupunguza gharama kiasi kinachosababisha kiwanda kupata faida na kuwawezesha kufanya matumizi mengine ikiwa ni pamoja na kuongeza maslahi kwa watumishi wake.
“nawashauri wenye viwanda na wengine wenye matumizi makubwa waweze kufanya ukaguzi wa ufanisi wa nishati ili kuweza kuokoa gharama pamoja na kuongeza faida katika uzalishaji” aliongeza Bw.Mapunda.
Mpaka sasa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania(TIRDO) mbali na kuwa na maabara ya kisasa lakini pia wana wataalam wenye Ithibati wenye uwezo wa kufanya ukaguzi wa mifumo ya matumizi ya umeme ndani na nje ya nchi(Energy Audit), kushauri matumizi bora ya nishati pamoja na usimamizi endelevu wa matumizi bora(Energy Management).
0 Comments