Na. Alfred Mgweno (TEMESA)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa zaidi ya shilingi milioni 500 kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 kwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ajili ya ununuzi wa vitendea kazi vipya vitakavyotumika kwenye karakana za Wakala huo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mapema leo. Mhandisi Karonda amesema kwa mwaka jana pekee Serikali ilitoa zaidi ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kununua vitendea kazi.
''Kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha tunapata vitendea kazi vya kisasa ili tuendane na wakati na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yanajitokeza katika magari mapya yanayokuja sasa hivi.'' Amesema Mhandisi Karonda huku akiongeza kuwa Serikali pia inaendelea kuzifanyia ukarabati mkubwa karakana ikiwemo karakana ya Mkoa Arusha, Mtwara, Mara, Tabora, Kigoma huku karakana za Mikoa ya Tanga , Morogoro, Kagera zikitarajiwa kuanza kufanyiwa ukarabati hivi karibuni.
Mhandisi Karonda pia ameongeza kuwa Wakala huo kwa sasa uko kwenye mpango wa mabadiliko (Transformation Stratergy) ambao unalenga kuibadilisha TEMESA katika utendaji kazi wake ili kuweza kutoa huduma bora zaidi.
'' Miongoni mwa vitu ambavyo vipo katika huo mkakati mojawapo ni haya ambayo tumeanza kuyatekelea kwa mfano kuwa karibu na wateja wetu kufanya vikao vya wadau lakini pia kuweza kuingia makubaliano na wazabuni ambayo yatatusaidia kuweza kutoa huduma kwa haraka ili ule ucheleweshaji upungue, lakini pia vile vipuri ambavyo tutavipata viwe vina ubora unaokubalika kwa kuwa kuna dhamana sasa yule aliosambaza kile kipuri ana wajibika iwapo kile kipuri kitakuwa kina shida ya ubora na yote hiyo ni kutengeneza uwazi na uwajibikaji wa Taasisi yetu,'' amesema Mhandisi Karonda na kuongeza kuwa matarajio ya Wakala huo ni kutoa huduma nzuri ili mteja awe anahitaji kupata huduma TEMESA sio kwakuwa sheria inamtaka kufanya hivyo bali huduma nzuri anazozipata TEMESA ndio zimfanye aweze kufika TEMESA.
Aidha, Mkurugenzi pia ametoa angalizo kuhusu utaratibu na gharama za ukaguzi wa matengenezo ya magari yanayokwenda kukaguliwa katika karakana teule (gereji binafsi) ambapo amesema Wakala huo unayo miongozo ya matengenezo ya magari ambayo imetengenezwa kwa ajili ya kusimamia matengenezo ya magari.
''Tunao muongozo wa matengenezo ya magari uko wazi kwamba tuna karakana teule tunazofanya nazo kazi pale inapobidi kufanya hivo na utaratibu tumeuweka kwenye Sura ya Kwanza kifungu Namba 1.22 kifungu B ambacho kinaelezea utaratibu wa karakana hizo kwamba gari itakapokuja na kukubaliwa kupelekwa karakana teule, malipo atakayolipa mteja kwa TEMESA kwa ajili ya ukaguzi wa awali (Pre Inspection) na ukaguzi baada ya matengenezo kukamilika (Post Inspection) ni shilingi Laki moja na ishirini tu.'' Amesema Mhandisi Karonda na kutoa wito kwa wadau wote wanaotumia huduma za Wakala huo kutoa taarifa kwa Wakala kama kuna karakana yoyote teule inayochaji gharama kinyume na muongozo uliowekwa ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Mhandisi Karonda ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuiboresha TEMESA upande wa miundombinu, vitendea kazi pamoja na ujio wa watumishi wapya ambapo amesema hicho kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Wakala huo.
0 Comments