Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUTUMIA FEDHA NYINGI MAFUNZO YA VIJANA JKT, WATAKIWA KUISHI VIAPO VYAO.


Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulidi Surumbu akiwa jukwaani wakati vijana wakila kiapo cha utii.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe.Jokate Mwegelo akiongea na vijana waliohitimu mafunzo.

Mkuu wa kikosi 838 Maramba JKT, Kanali Ashraf Hassan akitoa taarifa ya kikosi operesheni miaka 60 ya JKT.
Vijana wa mujibu wa sheria operesheni miaka 60 ya JKT wakiimba kwa shangwe kabla ya kufungwa kwa mafunzo hayo.

Vijana wakipita na Gwaride mbele ya mkuu wa Wilaya Kanali Surumbu.

************************

Na Hamida Kamchalla, MKINGA.


VIJANA waliomaliza mafunzo ya awali ya kijeshi kwa mujibu wa sheri, kikosi 838 Maramba JKT, operesheni miaka 60 ya JKT wametakiwa kwenda kukiishi kiapo walichoapa kwa kulitumikia Taifa lao kiuzalendo.


Kupitia mafunzo hayo serikali inatumia fedha nyingi katika kuyaendeleza ili kupata vijana ambao watakuwa wazalendo kwa Taifa hivyo inawapasa kuyatumia vema mafunzo waliyopata na kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa vijana wenzao na hata wazazi ambao wanawazuia watoto wao kujiunga na mafunzo hayo.


Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulidi Surumbu ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo hayo ambapo alisisitiza vijana mbali na uzalendo wa nchi lakini pia mafunzo ya stadi za kazi waliyopatiwa yatasaidia kuwaletea maendeleo yao binafsi.


"Mzingatie mafunzo mliyopata kwa muda wote mliokuwa hapa, ili yaweze kuwa chachu ya maendeleo yenu binafsi pamoja na Taifa kwa ujumla, lakini pia mtambue kwamba Taifa lina matarajio makubwa sana kwenu na ndiomaana tunatumia fedha nyingi kuhakikisha mnapata mafunzo haya" amesema.


"Taifa likiwa na vijana wenye nguvu na moyo wa kuipenda nchi yao hata maendeleo na uchumi vinaimarika kwani vijana wenye uzalendo hulijenga Taifa lao kwa moyo mmoja" amebainisha Kanali Surumbu.


Naye mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amewaasa vijana hao na kusema kuwa baada ya kuhitimu mafunzo wana jukumu la kuilinda, kuitetea na kuitumikia nchi yao kwa jinsi itakavyotakiwa.


"Ni matarajio yangu kwamba vijana hawa wameiva vizuri na wakitoka hapa watakwenda kuwa mabalozi wazuri kule majumbani kwao kwa kile walichiojifunza lakini na kwa nchi yetu pia, mimi nimependa zile stadi za kazi kwa vijana hawa,


"Sasa hivi stadi za vijana wengi ni kushika simu na kuchati, lakini unapokuwa na za kazi kama hizi, utaweza kushika jembe na kulima bustani ya mbogmboga na kujipatia kipato, kwahiyo rai yangu kwenu vijana wenzangu, mna kazi kubwa ya kuisemea nchi yetu" amesisitiza Mwegelo.


Kwa upande wake mkuu wa kikosi 838 Maramba JKT, Kanali Ashraf Hassan amesema vijana hao walianza mafunzo rasmi juni 19 mwaka huu na walifanya ndani ya majuma 12 mfululizo ambapo pia waliweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni maelekezo kutoka makao makuu ya jeshi hilo.


"Vijana hawa kwa kipindi chote walichokaa hapa kambini walifundishwa masomo yaliyokusudiwa kwa kufuata mwongozo na silabi ya sheri ya mujibu wa vijana kutoka makao makuu, kupitia mafunzo yao pia vijana hawa sasa ni timamu na wanaelewa nini maana ya ulinzi wao binafsi na Taifa lao kwa ujumla" amesema.


Aidha vijana hao wamebainisha kwamba wana furaha kubwa kwa kupata mafunzo hayo kwani wameweza kujitambua na kujua nini maana ya uzalendo lakini pia wamekuwa timamu kwa kufuzu mafunzo ya awali ya kijeshi kwa kujifunza mambo mengi ambayo awali hawakuyafahamu.


"Tunamshukuru Mungu kwa kuhitimisha mafunzo haya ambayo yametujenga kiakili na kimwili pia, mimi nilikuwa nikisikia uzalendo tu lakini sikujua hasa maana halisi, sasa naondoka hapa nikiwa timamu, naahidi kwamba kiapo nilichokula kitaishi ndani yangu na niko tayari kuitumikia nchi yangu kwa vyovyote nitakacyoelekezwa" amesema, Amani Omari kutoka Gairo.


"Lakini pia tumejifunza kitu kikubwa sana katika maisha ambacho ni nidhamu, hapa tumekutana vijana wengi kutoka mikoa mbamimbali na kila mmoja ana tabia yake, lakini kupitia mafunzo haya watu wamenyooka, JKT sio linajenga taifa bali pia linatujenga sisi vijana kuwa wepesi wa kutekeleza maagizo" amesema.


"Tumejifunza uzalishaji mali na tumeelewa vema, tukitoka hapa naamini kama vijana kuna watakaoendelea vyuoni lakini bado tuna uwezo wa kujiajiri katika kilimo na ufugaji na tukajiongezea kipato, hivyo tunaishukuru serikali yetu kwa kutulea na kutupatia mafunzo haya" amesema Christina Humba.

Post a Comment

0 Comments