Na Hamida Kamchalla, TANGA.
VIJANA wawili raia wa nchi jirani ya Kenya wametiwa mbaroni na jeshi la polisi Mkoa wa Tanga wakifanya uhalifu wa kuiba na kupora fedha na vitu mbalimbali vya thamani katika maegesho ya magari huku wengine kadhaa wakihukumiwa kutumikia vifungo jela kulingana na makosa yao.
Raia hao wa Kenya waliingia nchini na kuanza kufanya matukio ambapo walikuwa wakivizia watu wanaotoka kuchukua fedha katika taasisi mbalimbali za fedha, hususani benki na wakiwa wanaondoka wao walifuata nyuma hadi eneo wanaposimama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi alisema watuhumiwa hao walikamatwa septemba 12 mwaka huu majira ya saa 3:30 asubuhi, mtaa wa barabara 13, jijini humo na kujitambulisha kwa majina ya Idrisa Mussa Kassim (24), fundi umeme na Samwel Kimati Mwenda (35) mfanyabiashara.
"Watuhumiwa hawa walikuwa wakitumia gari aina ya IST lenye rangi ya silver likiwa na namba T 931 CVS ambalo walilitumia kutekeleza uhalifu wao lakini pia baada ya kufanyiwa upekuzi walikutwa na rimoti tatu, moja ya kuzimia sauti, ya kufungulia magari yenye lock pamoja na ya kufungulia mageti" alisema.
"Vilevile walikutwa na simu tatu za smartphone pamoja na vitambulisho mbalimbali, walihojiwa na kukiri kufanya matukio kadhaa lakini kosa walilokamatwa nalo ni moja na litawafikisha mahakamani kwenda kujibu tuhuma zao" alisisitiza Kamanda Mchunguzi.
Aidha Kamanda alisema kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja wamefanikiwa pia kuwakamata watuhumiwa mbalimbali kutokana na matukio tofauti tofauti ikiwemo bangi, mirungi, pombe ya moshi (gongo) pamoja na pikipiki, ambapo watuhumiwa wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Hata hivyo Kamanda alibainisha kuwa vijana wanne wa jamii ya Kimaasai walioko kijiji cha Msomera wilayani Handeni wamefikishwa mahakamani kutokana na kujihusisha na wizi wa mifugo
"Vijana hao ni Taigwa Matapeli (26), Temi Makulea (23), Daeli Zakayo (24), Adam Yusuph (23), pamoja na Khalid Saidi, mkazi wa kijiji cha Mbangwi na watuhumiwa hawa wote tayari tumeshawafikisha mahakamani wakisubiri kujibu tuhuma zao zinazowakabili" alisema.
Kamanda Mchunguzi pia alitoa wito kwa wananchi wenye nia njema kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili liweze kuwa na taarifa nyingi zaidi za matukio ya kiuhalifu ndani ya Mkoa huo.
0 Comments