Ticker

6/recent/ticker-posts

MWAROBAINI WA WAVUVI HARAMU UMEPATIKANA ENEO LA UHUFADHI, MOA.



******************

Na Hamida Kamchalla, MKINGA.


KUFUATIA kuwepo kwa tatizo la vitendo vya uvuvi haramu na uchafuzi wa mazingira katika Pwani ya Bahari ya Hindi eneo la Moa, wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga wadau wa uhifadhi wa bahari na maeneo tengefu (MTRU) wamekuja na mwarobaini wa kukomesha vitendo hivyo.

Shirika la Jamii ya Uhifadhi wa Wanyamapori (WCS) limefanikiwa kuwajengea uwezo wadau hao katika eneo hilo kwa kuwapatia jengo la ofisi, gari na vifaa vya kufanyia kazi ambavyo vitawasaidia katika kupambana na vitendo vya kiharamia vinavyoendelea baharini.


Kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulidi Surumbu amesema ndani ya wilaya hiyo katika meneo ya pwani kulikuwa na tatizo kubwa la uvuvi haramu, lakini baada ya serikali kufanya misako ya mara kwa mara tatizo limepungua kwa kiasi kidogo kwani wapo watu ambao bado hawataki kuelewa.


"Sasa hivi tuna kila sababu ya kujipongeza kwakuwa majanga yamepungua sana, lakini bado hayajaisha, kwahiyo uwepo wa vifaa hivi sasa unakwenda kuongeza kasi ya kumaliza kabisa tatizo hili, kwahiyo salamu ziwafikie wale wasiotaka kubadilika" amesema Kanali Surumbu.


"Nitoe wito kwa wananchi wote wa wilaya ya Mkinga ambao wanaendeleza vitendo vya uchafuzi wa bahari wabadilike na waache kabisa, kwasababu vifaa vya kisasa vimekuja kuongeza nguvu na sasa hakuna kwa kujificha, kwahiyo niwaombe sana wananchi kuvitunza hivi vifaa kwa maslahi mapana ya nchi yetu" amesisitiza.


Aidha Kanali Surumbu amesema hifadhi ya mazingira ya bahari ni muhimu sana katika utunzaji wa rasilimali ya uvuvi, hususani katika mazingira yote yanapaswa kuzingatia kaulimbiu ya uvuvi, ambayo inazingatia mazingira


"Na kwa kutambua hili, serikali iliamua kuanzisha hifadhi ya bahari na maeneo tengefu kupitia sheria namba 29 ya mwaka 1994, kwa sasa maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa nchini yamefikia ukubwa wa km za mraba 2220, sawa na asilimia 6.5 ya bahari ya ndani" amefafanua Kanali Surumbu.


Naye Mkurugenzi mkuu wa WCS Simon Lugandu amesema malengo makubwa ya shirika hilo ni kufanya uhifadhi wamazingira kwa bayoanuai walizonazo lakini pia wanalenga katika kujikwamua kiuchumi na kwamba tayari wamekwishafanya miradi mingi katika Mikoa tofauti.


Lugandu amesema tangu kuanza kwa shirika hilo wameshatekeleza miradi ipatayo 150 ambapo mingi kati yake ilihusu utafiti na mingine ni ya uhifadhi, na katika misitu kazi yake ni kuhifadhi mali asili ya wanyamapori na kwa upande wa bahari wanahifadhi maliasili ya matumbawe na viumbe vilivyomo.


"Watanzania tuna bahati, takribani asilimia 40 ya maeneo tuliyonayo nchini yamehifadhiwa kwa njia moja au nyingine, kwahiyo tumefanya kazi kubwa katika kuhifadhi rasilimali tulizonazo na ni wajibu wetu, nasema hivi ili kuwaelezea msisitizo kama shirika la WCS, kwamba ni muhimu tukahifadhi rasilimali hizi kwa ajili yetu na vizazi vinavyokuja" amesema.


"Shirika letu linatekeleza wajibu wake kama sera ya nchi inavyotaka, kwahiyo tunapoongelea mikakati mbalimbali ya maendeleo, kazi yetu ni kutoa mchango katika utekelezaji wa sera hizo ambazo serikali yetu imeziandaa, lakini pia tuna wajibu wa Kimataifa wa kutunza rasilimali ambazo ni za kigeni",


"Kwahiyo tunafurahi kuona kwamba ushirikiano tunaopata kutoka serikalini ni mkubwa na tuna makubaliano maalumu juu ya uwepo wa shirika letu na kwa kifupi tuna mafanikio mengi ambayo tumeyapata katika utekelezaji wetu" amefafanua.


Kwa upande wake wa mradi wa Uhifadhi wa Bahari, Jean Mensa amesema kuwepo kwa uhifadhi wa bahari na maeneo tengefu ni muhimu sana kwani inaweza kuchangia katika sekta ya uvuvi, lakini pia katika umuhimu wa mazingira pamoja na kusimamia wananchi.


"Kwahiyo utengaji na uwekaji wa mipaka kwenye maeneo haya ni muhimu sana katika usimamizi lakini pia katika kuongeza na tekinolojia zitakazohusika katika usimamizi huo" amebainisha Mensa.

Post a Comment

0 Comments